KISA Yanga wachezaji Prisons wanyimwa Likizo, hiyo ni baada ya Kocha wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa kusema kikosi chake hakitakuwa na muda wa mapumziko katika kipindi ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa ajili ya kupisha FIFA Series.
Baada ya mapumziko hayo mafupi Tanzania Prisons atakuwa na kibarua cha kusaka alama tatu mbele ya Yanga katika mchezo wa ligi utakaopigwa uwanja wa KMC Complex Aprili 4, 2026.
Amesema badala yake kitaendelea na kazi ya ziada kwa lengo la kuboresha utulivu wa wachezaji wake wanapokuwa uwanjani.
Nsajigwa alikabidhiwa jukumu hilo kufuatia kuondoka kwa Zedekiah Otieno kutokana na matokeo yasiyoridhisha.
Tangu achukue usukani, tayari ameiongoza timu hiyo katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini bado hajafanikiwa kupata ushindi.
Katika michezo hiyo, Prisons ilipata sare dhidi ya Azam FC kabla ya kupoteza mbele ya Yanga kwa mabao 1-0 na baadaye kufungwa 2-1 na Singida Black Stars.
Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuendelea kubaki katika hali ngumu, ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.
Hadi sasa, Prisons imecheza mechi 17, ikishinda tatu pekee, sare nne na kupoteza michezo 10, hali iliyoifanya kukusanya pointi 13 tu. Takwimu hizi zinaonyesha wazi changamoto kubwa inayokikabili kikosi hicho msimu huu.
Nsajigwa ameeleza kuwa moja ya matatizo makubwa ni kukosekana kwa utulivu kwa wachezaji wanapokuwa ndani ya uwanja, jambo linalosababisha kufanya maamuzi yasiyo sahihi katika nyakati muhimu za mchezo.
Amesisitiza kuwa utulivu ni jambo la msingi katika mafanikio ya timu yoyote, huwasaidia wachezaji kucheza kwa umakini na kufanya maamuzi sahihi hata wanapokuwa chini ya presha kubwa.
“Natumia kipindi hiki kuhakikisha wachezaji wanajengewa uwezo wa kiakili pamoja na nidhamu ya mchezo, ili waweze kubadilisha mwelekeo wa matokeo katika michezo ijayo,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa baada ya mapumziko, timu itarejea rasmi mazoezini ikiwa na malengo maalum ya kuboresha kiwango cha uchezaji, kuimarisha nidhamu na kuongeza ushindani ndani ya kikosi hicho.