Home Habari za michezo OKELLO AONYA UTAMU YANGA, AWEKA MALENGO MAKUBWA

OKELLO AONYA UTAMU YANGA, AWEKA MALENGO MAKUBWA

0

BAADA ya kufunga bao katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello, ameahidi kuendelea kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo katika mechi zijazo.

Okello, ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo akitokea Vipers SC ya Uganda, ameanza kuonesha kiwango kinachotarajiwa na wengi, huku mashabiki wakiamini nyota huyo sasa ameanza kuwaka.

Akizungumzia mchango wake katika mchezo huo, Okello amesema anafurahia kufunga bao pamoja na kuhusika katika bao la pili, akisisitiza kuwa ataendelea kupambana ili kusaidia timu yake kupata matokeo chanya.

“Nafurahi tumepata alama tatu mbele ya Tanzania Prisons. Pia kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi kunanipa hamasa na kunichochea kuendelea kupambana ili kuisaidia timu kupata matokeo mazuri,” amesema Okello.

Ameongeza kuwa ana imani kubwa na kikosi hicho kuendelea kupambana katika mechi zijazo, akilenga kuhakikisha wanakusanya alama tatu muhimu zitakazowaweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia lengo lao la kutwaa ubingwa pamoja na kuwapa furaha mashabiki wao.