BAADA ya kusuluhu mbele ya Azam FC, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema bado wana imani kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Ahmed amesisitiza kuwa matokeo hayo hayajabadili malengo ya timu, akieleza kuwa ligi ni mbio ndefu zinazohitaji uvumilivu na umakini mkubwa katika kila mchezo.
Amesema sare hiyo dhidi ya Azam FC haiwezi kuwa kikwazo kwao, bali ni sehemu ya ushindani wa kawaida, huku akiahidi kuwa wataendelea kupambana katika michezo ijayo ili kujikusanyia alama tatu muhimu.
“Tumekubali kwamba msimu huu Azam FC wamepata alama nne kutoka kwetu, baada ya kutufunga katika mzunguko wa kwanza na sasa kutoka sare, lakini hilo halijatuondolea imani ya kupigania ubingwa. Bado mechi nyingi zipo mbele yetu,” amesema.
Ameeleza kuwa mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa wapinzani wao, ambao walionesha kiwango kizuri uwanjani.
Ahmed amesema Simba walikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushinda, hasa katika kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo kutokana na kukosa utulivu wanapofika eneo la mwisho.
Ameongeza kuwa kikosi hicho kitajifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo, kurejea kikiwa imara zaidi katika mechi zijazo ili kuhakikisha wanabaki kwenye mbio za ubingwa hadi mwisho wa msimu.
Hadi sasa Simba imeshacheza michezo 16 ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kukusanya alama 35 wakiwa nafasi ya pili nyumq ya Yanga anayeongoza ligi hiyo akiwa na pointi 41 akucheza mechi 17.