Home Habari za michezo NZENGELI AIBEBA YANGA, WAPO TAYARI KWA VITA YA MWISHO

NZENGELI AIBEBA YANGA, WAPO TAYARI KWA VITA YA MWISHO

0

LICHA ya kuendelea kufanya vizuri na kutopoteza mechi katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB, kiungo wa Yanga, Max Nzengeli, amesema bado hakuna nafasi ya kupumzika kutokana na ushindani mkubwa uliopo, huku wakikabiliwa na wapinzani wagumu kila wanaposhuka dimbani.

Nzengeli ameeleza kuwa kadri ligi inavyoelekea ukingoni, presha ya ushindani inaongezeka, hivyo hawana budi kuingia kila mchezo kwa umakini mkubwa bila kudharau timu yoyote, bila kujali nafasi yake kwenye msimamo wa ligi.

“Ushindani wa ligi ni mkubwa na mashabiki wanahitaji kuona furaha kupitia matokeo mazuri. Sisi kama wachezaji tunalenga kuendelea kulinda rekodi yetu ya kutopoteza mechi,” amesema Nzengeli.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaweza kupatikana kwa nidhamu, kujituma na kuwaheshimu wapinzani wao kila wanapokutana nao uwanjani.

“Ili kufikia malengo yetu, tunapaswa kucheza kwa nidhamu na kumheshimu kila mpinzani. Kwa sasa kilicho muhimu ni timu; sisi tutaendelea kufanya kazi yetu na kupambana hadi mwisho,” ameongeza.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Alhamisi, Aprili 16, 2026, kuikaribisha Mbeya City katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya, timu hizo ziligawana alama moja baada ya kutoka sare, jambo linaloongeza ushindani kuelekea pambano hilo lijalo.