UONGOZI wa klabu ya Simba SC umeweka wazi hali ya kipa wao, Moussa Camara, kwa kueleza kuwa kwa sasa anasumbuliwa na majeraha na yupo chini ya uangalizi wa kitabibu.
Taarifa hiyo imekuja kufuatia sintofahamu iliyokuwa imeibuka miongoni mwa mashabiki kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi hicho.
Katika siku za hivi karibuni, kulikuwa na tetesi zikidai kuwa kipa huyo huenda asiongezwe mkataba wake pindi utakapomalizika mwishoni mwa msimu ujao. Taarifa hizo zilidai kuwa tayari baadhi ya wasimamizi wake wameanza kupewa ishara kuwa hatabaki ndani ya timu hiyo.
Hata hivyo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amekanusha uvumi huo na kusisitiza kuwa hali ya Camara ni ya kawaida kama ilivyo kwa wachezaji wengine waliopo kwenye majeruhi ndani ya kikosi hicho.
Ahmed aliwataja baadhi ya wachezaji wanaokabiliwa na changamoto kama hiyo kuwa ni pamoja na Yakubu Suleiman, Nickson Nangu na Abdulrazack Hamza, akieleza kuwa wote wana mikataba halali na wanaendelea kuhudumiwa hadi watakapopona.
Amefafanua kuwa kwa sasa hakuna uamuzi wowote uliofanyika kuhusu hatma ya Camara, bali kinachosubiriwa ni tathmini ya kitabibu itakayofanywa mwishoni mwa msimu ili kubaini kama ataweza kurejea kikosini au ataendelea na matibabu zaidi.
“Camara ni mchezaji wa Simba kwa sasa, na suala lake ni majeraha kama ilivyo kwa wengine. Tunasubiri hadi mwisho wa msimu ambapo madaktari watatoa tathmini ya hali zao,” amesema Ahmed, akisisitiza kuwa klabu ina utaratibu wa kufuata ushauri wa kitabibu kabla ya kufanya maamuzi yoyote.
Ameongeza kuwa wachezaji wote ambao watathibitika kuwa bado hawajapona wataendelea kupata matibabu hadi watakapokuwa tayari kurejea uwanjani, huku wale watakaopona wakitarajiwa kurejea kuisaidia timu katika majukumu yake ya mashindano yajayo.