MECHI sita mfululizo ilizocheza Mtibwa Sugar bila kuonja ushindi, imewaamsha nyota wa timu hiyo na kutangaza mkakati mpya wa kumaliza michezo 12 ya Ligi Kuu Bara iliyobaki.
Timu hiyo ambayo imerejea Ligi Kuu msimu huu, haikuwa na mwanzo mzuri kabla ya kubadilika na kujiweka nafasi ya tisa kwa pointi 23 na kuwapa matumaini ya kubaki salama msimu ujao.
Hata hivyo, timu hiyo iliyowahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka miwili mfululizo, 1999 na 2000, katika michezo sita ya mwisho haijaonja ushindi ikiwa ni sare tatu dhidi ya Coastal Union (1-1), Yanga (1-1) na Namungo (1-1) na kupoteza tatu dhidi ya Azam (3-0), Singida BS (3-1) na Mashujaa (3-1).
Kwa sasa ‘Wakata Miwa’ hao wa mkoani Morogoro, wanatarajia kushuka uwanjani Aprili 18, mwaka huu kuwafuata Fountain Gate, mchezo ambao utapigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ukiwa wa raundi ya 19.
Beki wa timu hiyo, Erick Kyaruzi, amesema kwa sasa ligi imebadilika kwakuwa wanakutana na makundi mawili tofauti ikiwa ni wenye kuwania ubingwa na kukwepa kushuka daraja.
Amesema kutokana na hali hiyo, wachezaji wamejipanga kwa mazingira yote kuhakikisha wanayekutana naye wanakomaa kupata pointi tatu ili kumaliza ligi katika nafasi nzuri bila presha ya kushuka daraja.
“Inapofika mechi za mwishoni kama hivi ligi huwa na ushindani zaidi, sisi Mtibwa Sugar tumejipanga kukabiliana na yeyote tunayekutana naye bila kujali anawania ubingwa au kushuka daraja kwakuwa tunayo malengo yetu,” amesema Kyaruzi.
Nahodha huyo aliyewahi kukipiga Kagera Sugar, aliongeza kuwa kwa sasa akili zipo katika mchezo dhidi ya Fountain Gate ambao wanafahamu uzito na umuhimu wake akieleza kuwa kiu yao ni ushindi.
“Kwanza mashabiki waamini timu yao haishuki daraja, tunahitaji kuona tunamaliza nafasi nzuri ambayo haitatupa presha kwa namna yoyote, tunaenda kwa tahadhari ili kufikia malengo yetu msimu huu,” amesema nyota huyo.