Home Habari za michezo KOCHA COASTAL HESABU KUBWA ZIPO LIGI KUU MENGINE BONASI

KOCHA COASTAL HESABU KUBWA ZIPO LIGI KUU MENGINE BONASI

0

BAADA ya kuwasha moto katika mechi mbili mfululizo, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema licha ya kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, lakini nguvu na hesabu kubwa zipo Ligi Kuu ili kuinusuru timu kutoshuka daraja.

Kocha huyo ambaye amerejeshwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Mohamed Muya, ameongoza mechi mbili akianza na Kombe la Shirikisho la CRDB kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Pamba Jiji na kutinga robo fainali.

Pia aliiongoza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda mabao 3-1 na sasa inajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Singida Black Stars itakayochezwa Mei 2, kabla ya kuvaana nao tena kwenye Shirikisho kusaka tiketi ya nusu fainali.

Akizungumza na Soka la Bongo, Elias amesema ameridhishwa na kiwango walichoonesha nyota wake akifichua kuwa siri kubwa ya kuanza vyema ni kutengeneza ushindani wa wachezaji wenyewe ndani na kuwapa nafasi kila mmoja.

Amesema mafanikio hayo ikiwamo kufuzu robo fainali ya kombe la shirikisho, lakini masharti aliypopewa ni kuitoa Coastal Union katika presha na mashaka ya kushuka daraja, lakini mengineyo ni bonasi kwake.

“Kikubwa niliambiwa niitoe timu kwenye mashaka na presha ya kushuka daraja, hivyo nguvu kubwa ipo Ligi Kuu, mengine yatakayokuja huko mbele kwangu ni bonasi tu, siri kubwa ni kuwaamini wachezaji na kutengeneza ushindani baina yao,” amesema Elias.

Kocha huyo ameongeza kuwa, baada ya matokeo mazuri aliyoanza nayo, mkakati ni kuendelea kuwapa makali mastaa wake kuhakikisha wanaishi na dhana ya ushindi kwa kila mchezo ili kuongeza ari na morali kwao.

Amekiri ligi kuwa ngumu haswa kwa mechi hizi za mwisho akieleza kuwa Coastal Union itapambana kadri iwezavyo kwa kila mchezo wanaokutana nao wanapambania pointi tatu bila kujali upinzani.

“Tunahitaji kulinda dhana hii ya kushinda kila mechi, inapotokea tukapoteza ni sehemu ya matokeo ya mpira ila tunahitaji kumaliza nafasi nzuri bila presha na niombe sapoti ya mashabiki,” amesema kocha huyo.