Home Habari za michezo MBEYA CITY YATUA KWA MAKOCHA WATATU KUMPATA MRITHI WA MAXIME

MBEYA CITY YATUA KWA MAKOCHA WATATU KUMPATA MRITHI WA MAXIME

0

WAKATI Mbeya City ikirejea jijini Mbeya kichovu baada ya kukutana na kipigo kizito dhidi ya Yanga, vikao vimeanza kwa mabosi wa timu hiyo kujadili ishu ya kocha mpya huku majina matatu yakiwaumiza vichwa kupata mmoja wapo.

Mbeya City ikicheza dhidi ya Yanga Aprili 16, 2026 katika Ligi Kuu Bara, ilikumbana na aibu ya kisago cha mabao 6-0 na kusababisha kibarua cha aliyekuwa Kocha Mkuu, Mecky Maxime kufikia tamati kwa pande zote kukubaliana kuachana.

Baada ya mchezo huo, timu hiyo ilirejea Mbeya kuendelea na maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa utakaopigwa Aprili 30, huku matarajio ikiwa ni kuendelea kutumia uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati kufuatia Sokoine uliopo Mbeya kutofunguliwa.

Maxime aliyeiongoza timu hiyo kwa mechi 12, ameshinda tano zikiwamo tatu za Kombe la Shirikisho la CRDB, sare tatu dhidi ya Pamba Jiji, Dodoma Jiji na Azam na kupoteza sita ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho CRDB dhidi ya Singida Black Stars walipolala 5-1.

Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na KMC, alikuwa kocha wa pili kufanya kazi kikosini humo akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Malale Hamsin ambaye naye alisitishiwa kibarua kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Habari za ndani ilizopata Mwanaspoti kutoka kwa mmoja wa vigogo wa timu hiyo ni kuwa, kwa sasa wanaendelea kujadili kumpata kocha mpya na benchi zima la ufundi ambaye ataingia na matokeo mazuri.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa, licha ya kwamba hawajafikia muafaka, lakini makocha wanaotajwa ni Mohamed Ismail ‘Laizer’ aliyeachana na Fountain Gate hivi karibuni, Mohamed Muya aliyeachana na Coastal Union na Mbwana Makata anayeinoa Polisi Tanzania ya Championship.

“Bado hatujaamua nani aingie kutegemeana na mapendekezo ya viongozi, lakini tunahitaji kocha ambaye anakuja kufanya kazi kutupa matokeo na kutuacha katika malengo yetu tuliyojiwekea.

“Vikao ndio vimeanza, kwahiyo huenda kuanzia Jumatatu wakati wa mazoezi ya wachezaji yatakapoanza tunaweza kuwa tumefikia muafaka na mmojawapo kati ya majina hayo, muda utaongea,” amesema kigogo huyo.

Ameongeza kuwa, kwa sasa timu inatarajia kuendelea na mazoezi Jumatatu kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mashujaa akieleza kuwa mkakati wao ni kufanya vizuri akitoa hofu mashabiki kutokata tamaa kwamba timu haishuki daraja.