Home Habari za michezo CHELSEA DUH TATIZO NI HILI KOCHA MPYA ATAJWA

CHELSEA DUH TATIZO NI HILI KOCHA MPYA ATAJWA

0

LONDON, ENGLAND: MCHAMBUZI na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya England na Manchester United, Gary Neville ameikosoa vikali bodi ya Chelsea kutokana na uamuzi wao wa kumfuta kazi Kocha Liam Rosenior, akieleza tatizo ni wao na sio yeye.

Ingawa gwiji huyo wa Man United hakusema moja kwa moja kuwa Rosenior alipaswa kubaki, alisisitiza mfululizo wa maamuzi mabaya ya uongozi ndiyo umeifikisha klabu hapo ilipo sasa.

Akizungumza na Sky Sports, Neville amesema: “Sioni kabisa sera wala mpango wa Chelsea. Mikataba ya miaka sita au nane wanayotoa  iwe kwa kocha au mchezaji ni ya kuchekesha tu.”

“Wamiliki hawajui wanachofanya. Nimewahi kufanya makosa kama mmiliki na wakati mwingine unapaswa kukubali hujui unachofanya. Sielewi kabisa. Kwenye soka, unapata unachostahili  na hilo linawahusu wamiliki, si kocha.”

Wamiliki wa klabu hiyo, Todd Boehly na Behdad Eghbali, tayari wametumia zaidi ya Pauni 1.5 bilioni  kusajili wachezaji, na wameshaajiri na kufukuza makocha sita hadi sasa.

Neville pia aliwakosoa baadhi ya wachezaji, akiwataja Marc Cucurella na Enzo Fernández kwa kauli zao za hivi karibuni, akidai zimeongeza presha kwa Rosenior.

“Wao ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye uzoefu, lakini walimuweka kwenye wakati mgumu kwa kuonyesha wazi wanamkubali zaidi Enzo Maresca, wakati hata chini yake hawakuwa wanafanya vizuri sana,” amesema.

Kuhusu Rosenior mwenyewe, Neville alieleza huenda alipewa nafasi hiyo mapema sana:”Labda hakupaswa kupewa nafasi hiyo mapema hivyo. Alipaswa kuendelea kujijenga kama kocha kijana mwenye kipaji.”

Hata hivyo, alikiri kuwa ilikuwa vigumu kwa Rosenior kukataa nafasi hiyo:

“Naelewa huwezi kukataa kazi ya Chelsea. Ni nafasi kubwa sana. Lakini sasa anapaswa kuendelea na kazi yake ya ukocha na kuachana na yaliyopita haraka iwezekanavyo.”

Kwa jumla, Neville anaamini kuwa matatizo ya Chelsea yanatokana na maamuzi yasiyo thabiti ya uongozi tangu kuingia kwa wamiliki wapya kampuni ya BlueCo mwaka 2022, hali inayofanya klabu hiyo ionekane kukosa mwelekeo sahihi kwa sasa.

Kwa sasa makocha kadhaa wametajwa wanaweza kuchukua mikoba ya Rosenior, lakini Andoni Iraola ndio anapewa nafasi kubwa kwa sasa.

Haijafahamika ikiwa mazungumzo ramsi na wakala wake yameshaanza lakini katika majina ya wenye asilimia nyingi za kupata kazi yeye ndio anaonekana kuwa namba moja kutokana na kazi kubwa aliyoifanya akiwa na Bournemouth licha ya kutokuwa na wachezaji wengi wenye ubora mkubwa.

Kwa sasa Chelsea inanolewa na Kocha Calum McFarlane ambaye ni kocha wa timu ya vijana ya U-21 na ndio alihudumu katika mechi mbili kabla ya Rosenior kuanza kazi rasmi.

Kazi ya kjwanza ya McFarlane itakuwa ni Jumapili ya wiki hii dhidi ya Leeds United katika nusu fainali ya Kombe la FA.