Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu amerejea nchini akitokea Marekani alikokwenda kushiriki mbio za Boston Marathon, huku akisema siri ya kufanya vizuri inatokana na jitihada ambazo amekuwa akifanya kwa kushirikiana na wenzake kwenye mazoezi na pia namna ya kumaliza mbio.
Mbio hizo zilifanyika Aprili 20, 2026 jijini Boston ambapo Simbu alimaliza wa pili akitumia saa 2:02:47 na kuwa Mtanzania wa pili kumaliza mara mbili mfululizo mbio hizo akifanya hivyo, huku mwaka jana akimaliza kwa saa 2:05:04.
Mwingine ni Juma Ikangaa aliyemaliza mara tatu mfululizo 1988, 1989 na 1990 ilihali Gabriel Geay alimaliza nafasi kama hiyo 2023 kwa saa 2:06:04.
Simbu pia anakuwa Mtanzania pekee hadi sasa ambaye ametumia muda mfupi zaidi Boston Marathon akivunja rekodi yake ya mwaka jana kwa dakika mbili na sekunde 47 ambapo alikimbia saa 2:05:04.
Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Simbu amesema mbio hazikuwa rahisi kutokana na ushindani uliokuwepo dhidi ya wanariadha wengine walioshiriki hasa John Korir kutoka Kenya ambaye alitetea ubingwa na Benson Kipruto aliyemaliza wa tatu.
“Ukiangalia Benson ni mkimbiaji mkubwa na mzoefu sana, na ni mtu ambaye ameshinda mashindano mengi sana. Wakati alivyoondoka John Korir tukabaki na yeye hata kule njiani ilikuwa ni msuguano mkali sana kila mtu anataka kwenda,” amesema Simbu.
“Lakini nikasema huyu jamaa ngoja nimsubiri subiri, na nimekuwa bora sana kumaliza. Zilipobaki mita 200 nikaongeza spidi na nikaenda kiukweli, mbio sio rahisi lazima tuongeze bidii,” amesema Simbu.
Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya Utimamu wa Mwili na Michezo iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha, Kanali John Nyanchoa amempongeza Simbu kwa jitihada za kuitangaza nchi kimataifa kupitia michezo.
Amesema Simbu ni mtu ambaye anajituma, mwaminifu na mwadilifu jambo ambalo limemfanya aendelee kung’ara katika mashindano mbalimbali anayoshiriki ikiwemo kushinda pia medali ya dhahabu ya dunia mwaka jana.
Meja Didas Msholwa ni Mkuu wa kikosi 977 anapofanyia kazi Simbu, amesema ushindi huo ni wa Tanzania na kuongeza kuwa utii wake na kukubali kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi ndio siri ya mafanikio yake.
“Alituhakikishia atakwenda kufanya vizuri na kweli amefanya vizuri. Kwa hiyo ushindi wake umeleta chachu sana katika timu,” amesema Msholwa.
Kwa upande wake Moses Simon, mkurugenzi wa Ntua Communications inayosimamia chapa ya Simbu, amesema haikuwa rahisi kwa nyota huyo kupenya kutokana na njia ambayo ilikuwa inatumika, lakini kilichombeba ni maandalizi mazuri ambayo waliyafanya.