KIPA wa Simba SC, Moussa Camara, amevunja ukimya na kufunguka kuhusu changamoto ya majeraha aliyopitia, akisema hali hiyo inaweza kumrudisha nyuma mchezaji katika kufikia malengo yake ya kikazi.
Nyota huyo ameanza kuonyesha dalili njema za kurejea uwanjani baada ya kipindi kigumu kilichomuweka nje kwa muda, hatua ambayo imezua matumaini mapya ndani ya kikosi cha Simba na kwa mashabiki wake.
Kupitia picha alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Camara ameonekana akiwa gym akifanya mazoezi ya kuimarisha mwili wake. Hii ni ishara wazi kuwa safari yake ya kurejea kwenye ubora imeanza kushika kasi na anaendelea kupambana kila siku.
Katika ujumbe wake, Camara ameeleza kwa hisia kuwa majeraha yanaweza kumtenganisha mchezaji na kile anachokipenda zaidi, lakini kwa uvumilivu, ujasiri, msaada wa watu wa karibu pamoja na matibabu sahihi, bado kuna nafasi ya kurejea uwanjani akiwa imara zaidi.
Kauli hiyo imebeba uzito wa mapambano aliyopitia, huku pia ikionesha imani yake kubwa ya kurejea kwenye kiwango chake cha juu na kuendelea kuwa nguzo muhimu ndani ya kikosi chake.
Kipa huyo ameambatanisha ujumbe wake na neno “Alhamdulillah”, akionesha shukrani kwa hatua aliyofikia katika safari yake ya kupona na kuendelea kusonga mbele hatua kwa hatua.
Camara anaendelea na programu maalum ya mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili, huku akiwa na morali ya juu na hamasa kubwa ya kurejea langoni kuwatumikia Simba SC kwa ubora aliouzoea.