UONGOZI wa klabu ya Simba umeanza kuweka mikakati ya usajili kwa msimu ujao, ambapo sasa umeingia kwenye mpango mbadala (plan B) wa kumsaka mshambuliaji Kevin Bakare endapo watashindwa kumpata Souleyman Fofana.
Wachezaji hao wawili wote wanaitumikia klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ambapo wamekuwa wakionyesha ubora mkubwa katika safu ya ushambuliaji, hali inayowafanya kuwa miongoni mwa majina yanayovutia macho ya Simba kuelekea dirisha kubwa la usajili.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, Simba bado haijakata tamaa ya kumsajili Fofana ambaye ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa amefunga mabao 14 katika ligi ya Ivory Coast. Hata hivyo, endapo dili hilo litakwama, macho ya mabosi wa Simba yatageukia kwa Bakare kama mbadala wake wa moja kwa moja.
“Kwa sasa bado wanapambana kuhakikisha wanampata Fofana, lakini kama ikitokea wakamkosa, basi tayari wanaangalia uwezekano wa kumchukua Bakare ambaye pia yupo ASEC Mimosas,” amesema mtoa taarifa huyo.
imeelezwa kuwa Bakare ndiye mshambuliaji wa pili kwa ubora katika kikosi hicho, akiwa amefunga mabao nane na kutoa pasi tatu za mabao (assist), jambo linaloimarisha nafasi yake kuwa chaguo sahihi la pili kwa Simba.
Uongozi wa Simba umebainika kuwa makini katika usajili huo, ukipitia kwa kina majina yote yaliyopendekezwa na benchi la ufundi chini ya kocha Steve Barker, ili kuhakikisha kikosi kinakuwa imara zaidi kuelekea msimu ujao wa mashindano.