BENCHI la ufundi la Yanga SC, linaloongozwa na Kocha Pedro Goncalves limeanza vita ya kimbinu mapema zaidi kabla ya mpambano wa nusu fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Azam FC, kwa kufanya upelelezi wa kina ambao umewapa picha kamili ya wapinzani wao.
Kocha, Pedro akiwa na msaidizi wake Mathew Silva, walijitokeza katika uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar kushuhudia kwa macho yao mchezo wa robo fainali kati ya Azam FC na KVZ .
Uwepo wao haukuwa wa kawaida, bali ulikuwa sehemu ya maandalizi ya kimkakati yaliyojengwa kwa umakini mkubwa kwa ajili ya kuwasoma wapinzani wake wanakutana nao kwenye nusu fainali ambao ni Azam FC.
Katika dakika zote 90 za mchezo huo, macho ya benchi la Yanga yalikuwa kazini. Walichambua kila kipengele, kuanzia namna Azam inavyojenga mashambulizi, uimara wa safu yao ya ulinzi, hadi maeneo yanayoweza kuleta mwanya wa kiufundi.
Kwa maana ya kiushindani, Azam FC tayari imewekwa kwenye karatasi ya uchambuzi kabla ya kupigwa filimbi ya nusu fainali. Pedro Goncalves amesema maandalizi yao yako katika kiwango cha juu.
“Tunafahamu umuhimu wa mchezo huu. Ni nusu fainali, hakuna nafasi ya makosa. Tumefanya maandalizi ya kina na kikosi kiko tayari kiakili na kimwili,” amesema kocha huyo.
Hatua hiyo ya Yanga kwenda moja kwa moja uwanjani kuchunguza wapinzani wao inaonyesha jinsi wanavyolichukulia kwa uzito pambano hilo. Badala ya kusubiri taarifa za watu wa pembeni, walichagua kushuhudia wenyewe kila kitu kinachoendelea, jambo linaloongeza presha ya kimbinu kwa upande wa Azam FC.
Sasa macho na fikra zote zinahamia kwenye pambano la kesho saa 2:15 usiku. Yanga SC wanaingia wakiwa na taarifa kamili ya mpinzani wao, huku Azam FC wakikabiliwa na changamoto ya kukutana na timu iliyo tayari kwa kila hali ya mchezo.