Home Habari za michezo SINGIDA BLACK STARS YAREJEA DAR, YAJIPANGA UPYA BAADA YA PIGO MUUNGANO

SINGIDA BLACK STARS YAREJEA DAR, YAJIPANGA UPYA BAADA YA PIGO MUUNGANO

0

BAADA  ya kuondolewa katika michuano ya Kombe la Muungano na Mlandege SC, kikosi cha Singida Black Stars kinarejea Dar es Salaam kuanza maandalizi ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.

Singida Black Stars wanatarajiwa kuvaana na Coastal Union ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Mei 2, 2026 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, msemaji wa klabu hiyo, Hussein Massanza amesema kuwa timu yao imepata funzo kubwa baada ya matokeo ya Kombe la Muungano na sasa wanajipanga kurekebisha makosa yaliyojitokeza.

“Kuondolewa katika Kombe la Muungano ni pigo, lakini ndio uzuri wa mashindano. Mechi dhidi ya Mlandege haikuwa rahisi. Tunaondoka Zanzibar tukiwa na funzo kubwa sana kama timu,” amesema Massanza.

Ameongeza kuwa benchi la ufundi litaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana ili kuhakikisha wanakuwa bora zaidi kuelekea mechi zao zijazo za ligi.

“Tunaenda kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kabla ya mchezo wetu ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union. Tunajipanga vizuri,” ameongeza.

Pamoja na matokeo hayo, Massanza amesema lengo la klabu bado halijabadilika, kwani wanaendelea kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku pia wakiwa kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

“Tunaendelea kupigania malengo yetu. Baada ya kutoka Zanzibar tutaweka kambi Dar es Salaam na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuelekea Tanga kwa mchezo wetu ujao,” amesema .