Home Habari za michezo UZINDUZI FILAMU YA MICHAEL JACKSON WATABIRIWA MAKUBWA

UZINDUZI FILAMU YA MICHAEL JACKSON WATABIRIWA MAKUBWA

0

LEO Aprili 24 macho na masikio yapo Marekani kwenye uzinduzi wa filamu ya wasifu wa Mfalme wa Pop duniani, Michael Jackson huku ikitabiriwa kuweka rekodi ya mauzo.

Filamu hiyo iliyoigizwa na mhusika mkuu Jaafar Jackson, mpwa wa mwanamuziki huyo, imeanza kuvuta hisia za mashabiki hata kabla ya kuingia rasmi sokoni, huku wachambuzi wa soko la filamu wakitabiri mapokezi makubwa katika wiki ya kwanza.

Kwa mujibu wa makadirio ya vyombo vya uchambuzi wa burudani kama Deadline na Variety, filamu hiyo inatarajiwa kuingiza kati ya Dola65  milioni hadi 70 ambayo ni zaidi ya Bilioni 170 za Kitanzania kwa wiki ya kwanza na kuivunja rekodi iliyowekwa na filamu ya muziki ya Bohemian Rhapsody iliyoingiza Dola51  milioni mwaka 2018.

Filamu hiyo imeongozwa na Antoine Fuqua na kuandikwa na John Logan, ikimshirikisha pia Nia Long, Miles Teller na Colman Domingo.

Michael  inaelezea safari ya maisha ya nyota huyo kuanzia utotoni, kufanikiwa kwake na kundi la Jackson 5 hadi kuwa mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa duniani kupitia albamu zake maarufu kama ‘Off The Wall’ na ‘Thriller’.

Kwa upande wa mapokezi, trela iliyoachiwa mapema ilivutia watazamaji ndani ya muda mfupi mara tu ilipoachiwa mtandaoni, huku mitandao ya kijamii ikijaa maoni chanya kuhusu namna Jaafar Jackson alivyoonekana kufanana kwa karibu na mjomba wake.

Wengi walivutiwa na uigizaji wake, hasa katika vipande vilivyoonesha mitindo ya dansi na sauti inayokaribiana na ya Michael Jackson, jambo lililoongeza matarajio ya filamu hiyo.

Hata hivyo, pamoja na sifa hizo, kuna mjadala kuhusu namna trela ilivyogusa maisha binafsi ya msanii huyo.

Baadhi ya wachambuzi walieleza trela inaonekana kulenga zaidi mafanikio na umaarufu wake kuliko changamoto na tuhuma zilizowahi kumkabili, jambo lililozua mijadala kuhusu uwiano wa simulizi ya filamu hiyo.