BENCHI la ufundi na wachezaji wa Mlandege SC wameweka wazi kuwa wana majibu ya kuwapa wapinzani wao, Simba SC, watakapokutana katika nusu fainali ya Kombe la Muungano. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumamosi, Aprili 25, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia ya timu hizi mbili, huku mshindi akijihakikishia tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo. Hali hiyo inaongeza presha na hamasa kwa kila upande kuonyesha ubora wao uwanjani.
Kwa upande wa Simba SC, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, amesema kikosi chao kinaingia kwenye mchezo huo kikiwa na kumbukumbu ya maumivu ya mwaka 2024, walipopoteza ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa bao 1-0 na Mlandege SC.
Ameeleza kuwa matokeo hayo bado yapo akilini mwao na yamekuwa chachu ya kuongeza ari kwa wachezaji, wakilenga kufanya vizuri zaidi katika mechi hii muhimu ya nusu fainali.
Ahmed amesisitiza kuwa Simba haiingii uwanjani kwa lengo la kulipa kisasi, bali kutafuta majibu ya kilichotokea kwenye fainali hiyo na kuthibitisha ubora wao dhidi ya wapinzani hao.
“Tunawakumbuka walivyotufunga kwenye fainali ya Mapinduzi. Safari hii tunaenda kucheza nao tukiwa na malengo yetu, si kisasi, bali tunataka kujua walitufungaje,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa ana imani kubwa na kikosi chao, akisisitiza kuwa ubora waliokuwa nao unawapa nafasi nzuri ya kufikia ndoto ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano msimu huu.