HISTORIA YA MVUTO, UBABE NA VISASI
PAMBANO kati ya Azam FC na Yanga halipo tu ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, bali hata kwenye michuano mingine limekuwa likitoa burudani ya hali ya juu, ushindani mkali na kumbukumbu zisizosahaulika kwa mashabiki wa soka nchini.
Kila wanapokutana nje ya ligi, historia inaonyesha mechi zao zimejaa presha, mbinu kali na mara nyingi kuamuliwa kwa njia ya penalti.
Katika Kombe la Kagame, timu hizi zimewahi kukutana mara mbili zenye kumbukumbu tofauti. Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika fainali ya mwaka 2012, wakionesha ubora wao mkubwa.
Hata hivyo, mwaka 2015 Azam FC walilipiza kisasi baada ya kutoka sare tasa na kushinda kwa penalti 5-3 katika hatua ya robo fainali, wakionesha uimara wao katika matuta ya mwisho.
Mapinduzi Cup imekuwa uwanja mwingine wa vita kati ya miamba hii miwili. Azam FC wameonekana kuwa na makali zaidi katika michuano hiyo, wakishinda mechi kadhaa zikiwemo ushindi wa mabao 3-0 mwaka 2012 na ushindi mwingine mkubwa wa 4-0 mwaka 2017.
Pia waliwahi kushinda 3-0 mwaka 2019, wakidhihirisha ubabe wao. Hata hivyo, Yanga nao hawakuwa nyuma, wakifanikiwa kushinda baadhi ya mechi kupitia penalti, jambo linaloonyesha ushindani wao kuwa wa karibu na usiotabirika.
Katika Ngao ya Jamii, Yanga wamekuwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya Azam FC. Wamefanikiwa kushinda fainali kadhaa, zikiwemo za mwaka 2013 na 2014 kwa mabao 1-0 na 3-0 mtawalia.
Pia waliibuka na ushindi wa penalti mwaka 2015, kabla ya kuendeleza ubora wao kwa ushindi wa 4-1 katika fainali ya mwaka 2024. Hii inaonesha namna Yanga wanavyoweza kupanda kiwango katika mechi kubwa.
Michuano ya Kombe la Shirikisho nayo haikubaki nyuma katika ushindani huu. Yanga waliibuka mabingwa wa ASFC mwaka 2023 baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, na mwaka 2024 wakarudia tena ubabe huo kwa kushinda kwa penalti 6-5 katika fainali ya Kombe la CRDB, baada ya sare tasa ndani ya dakika 90.
Mbali na mashindano rasmi, hata katika mechi maalumu za hisani, timu hizi zimeendelea kuonyesha ushindani mkubwa. Mfano ni mwaka 2011 ambapo Azam FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa kuchangia watu wenye ulemavu, wakionesha kuwa hata nje ya mashindano makubwa, hakuna anayependa kupoteza mbele ya mwenzake.
Historia ya Azam FC na Yanga nje ya Ligi Kuu inaonyesha wazi kuwa huu si ushindani wa kawaida. Ni vita ya heshima, ubora na kujidhihirisha kila timu inapopata nafasi. Matokeo yao yamekuwa yakibadilika mara kwa mara, lakini jambo moja linalobaki ni kwamba kila wanapokutana, mashabiki hupata burudani ya hali ya juu na mechi zenye presha kubwa hadi dakika ya mwisho.