KUELEKEA mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Muungano kati ya Simba dhidi ya Mlandege SC, Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Steve Barker, amesema anatarajia kufanya mabadiliko ya kikosi kuelekea pambano hilo litakalopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Barker ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo muhimu, akisisitiza maandalizi yao yamekamilika kwa kiwango kinachoridhisha, huku lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata matokeo chanya yatakayowapeleka fainali.
Kocha huyo ameongeza kuwa wachezaji wake wote wako katika hali nzuri ya ushindani na wana morali ya juu, jambo linalompa imani kuwa kila mmoja yuko tayari kutoa kiwango bora uwanjani ili kutimiza malengo ya timu hiyo.
Pamoja na kujiamini huko, Barker amekiri kuwa wanakutana na timu imara yenye mafanikio makubwa visiwani Zanzibar, hivyo wanapaswa kuwa makini katika kila dakika ya mchezo huo.
Amesisitiza kuwa hawatachukulia mechi hiyo kirahisi, badala yake wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa wakilenga kutumia vyema nafasi watakazozipata ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Barker amebainisha kuwa nidhamu ya mchezo, umakini na utekelezaji sahihi wa maelekezo ya benchi la ufundi vitakuwa mambo muhimu yatakayoamua hatima ya mchezo huo, huku akiwataka wachezaji wake kujituma na kuonyesha ubora wao.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona ni nani ataibuka mshindi na kufuzu fainali ya Kombe la Muungano.