Home Habari za michezo JAMES MLANGE, KILA MECHI KWANGU NAFASI YA KUWEKA REKODI

JAMES MLANGE, KILA MECHI KWANGU NAFASI YA KUWEKA REKODI

0

MSHAMBULIAJI wa Fufuni, James Mlange amesema amejisikia vizuri kufunga hat trick katika mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya Junguni, huku akipanga kuweka rekodi msimu huu.

Mchezo huo uliochezwa Aprili 18, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, Fufuni iliibuka na ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Junguni, huku James akitupia matatu ‘hat trick’.

Akizungumza na Soka la Bongo kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Ndugukitu Machomanne, Wilaya ya Chakechake, kisiwani Pemba, amesema kati ya mabao hayo, la pili lilikuwa bora zaidi upande wake.

“Kilichonifanikisha zaidi kwenye mechi hiyo ni kujituma na kufuata maelekezo ya mwalimu kabla na baada ya mchezo,” amesema mshambuliaji huyo.

James amesema kwa kawaida kila mechi anajiandaa kufunga mabao kwa ajili ya timu akiamini yatamuweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa mfungaji bora.

Amesema mwalimu anapompa nafasi ya kucheza, anajitahidi kuonyesha alichonacho kumfurahisha na kuendelea kumuamini.

James alijiunga na Fufuni dirisha dogo la usajili msimu huu na hadi sasa amefunga mabao manane, hali inayomfanya kutajwa kama miongoni mwa washambuliaji hatari katika ligi hiyo.