Home Habari za michezo MWALIMU AAPA KUMSAKA DUBE HADI TONE LA MWISHO

MWALIMU AAPA KUMSAKA DUBE HADI TONE LA MWISHO

0

LICHA ya kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri kwenye mashindano, mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu, amesema kasi yake ya kufumania nyavu inampa changamoto mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, katika mbio za ufungaji bora.

Mwalimu ameeleza kuwa katika mechi tatu alizocheza tayari amefunga mabao mawili, huku mpinzani wake akiwa na mabao matatu. Hali hiyo imempa hamasa ya kuongeza juhudi ili aweze kumfikia Dube, hasa kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano.

Fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumatano, Aprili 29, 2026, ambapo Simba itakutana na Yanga kwenye dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Amesisitiza kuwa malengo ya kila mshambuliaji si tu kusaidia timu kupata ushindi, bali pia kuhakikisha anatumia kila nafasi anayopata kufunga ili kuwania tuzo ya ufungaji bora wa mashindano.

“Nimpongeze Dube kwa juhudi anazozifanya kwa klabu yake, lakini hata mimi kama mchezaji mzawa nipo tayari kumpa changamoto katika mbio za ufungaji bora,” amesema Mwalimu.

Ameongeza  kuwa mchezo wa Kariakoo Derby hautakuwa rahisi kutokana na ukubwa wake, akieleza kuwa mechi za aina hiyo huwa na presha na mbinu za kipekee zinazoweza kuamua matokeo.

Amesema  licha ya maneno yanayoendelea nje ya uwanja, lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanapambana hadi mwisho ili kutwaa taji la Kombe la Muungano.