Home Habari za michezo PEDRO AINGIA VITANI, AWACHAMBUA SIMBA KIPINDI KWA KIPINDI

PEDRO AINGIA VITANI, AWACHAMBUA SIMBA KIPINDI KWA KIPINDI

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves ameanza rasmi kazi nzito ya kujiandaa na mpinzani wake Simba, kwa kujikita katika uchambuzi wa kina wa mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Muungano.

Lengo kubwa likiwa ni kubaini mbinu na mifumo iliyotumika ili kupata mwanya wa kuwazidi wapinzani hao.

Hatua hiyo imekuja baada ya benchi la ufundi la Yanga, likiongozwa na wasaidizi wake Abdulhamid Moalin na Patrick Mabedi, kushuhudia kwa karibu mchezo wa nusu fainali kati ya Simba na Mlandege SC uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Katika uchambuzi huo, Moalin na Mabedi walifuatilia kwa umakini dakika zote 90 za mchezo huo, wakijikita zaidi katika kuelewa mfumo na mbinu za kocha wa Simba, Steve Barker, hususan namna alivyochezesha kikosi chake katika vipindi viwili tofauti vya mchezo.

Kipindi cha kwanza cha dakika 45, Simba walionekana kucheza kwa tahadhari zaidi, huku Barker akionekana kuficha baadhi ya mbinu zake muhimu, jambo lililoifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa sare ya bila kufungana (0-0).

Hata hivyo, sura ya mchezo ilibadilika kabisa katika kipindi cha pili, ambapo Barker alifanya mabadiliko muhimu ya wachezaji yaliyoleta uhai mpya ndani ya kikosi chake na kuongeza kasi ya mashambulizi.

Wachezaji walioingia akiwemo Yusuph Kagoma, Clatous Chama, Selemani Mwalimu pamoja na Anicet Oura walikuwa na mchango mkubwa katika kugeuza mwelekeo wa mchezo, hali iliyosababisha Simba kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mlandege.

Sasa jukumu kubwa linabaki kwa Pedro Goncalves kutumia taarifa na uchambuzi huo kwa ufanisi, hususan kwa kuangalia namna ya kukabiliana na mbinu za Simba katika vipindi vyote viwili vya mchezo, ili kuhakikisha Yanga inakuwa na makali ya kutosha kuelekea fainali inayosubiriwa kwa hamu kubwa.