Home Habari za michezo WIKI YA MOTO KWA SIMBA, YANGA WATINGA KWENYE MTEGO

WIKI YA MOTO KWA SIMBA, YANGA WATINGA KWENYE MTEGO

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana kwa ajili ya makombe, kikitambua kuwa kina nafasi muhimu ya kuwania taji katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuchezwa Jumatano.

Simba imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Muungano, ambapo itakutana na watani wao wa jadi Yanga katika mchezo utakaopigwa Aprili 29, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Barker amesema kuwa hii ni wiki muhimu kwa timu yake, kwani baada ya fainali hiyo ya Jumatano, watakutana tena na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili, Mei 3, 2026.

Kocha huyo ameeleza kuwa kwa sasa wanachukua hatua moja baada ya nyingine, wakianza na kufurahia ushindi walioupata, kabla ya kuelekeza nguvu zao zote kwenye maandalizi ya fainali.

“Leo tutakaa na kupanga mipango ya mechi ya Jumatano. Tupo hapa kushindana na kushinda mataji, sisi ni Simba, na hii ni nafasi nyingine ya kuwania ubingwa, hivyo lazima tujiandae vizuri. Kwa sasa hatuna mawazo ya mechi ya Jumapili,” amesema Barker.

Ameongeza kuwa mkakati wao ni kuzingatia kila mchezo kwa wakati wake, ambapo baada ya kumaliza fainali ya Jumatano, watahamishia nguvu zao kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, maarufu kama Kariakoo Derby.