MILAN, ITALIA: WAKATI mwamuzi mwamuzi wa zamani, Gianluca Rocchi, akijisimamisha kwa hiari kutoka nafasi yake ya bosi wa waamuzi nchini Italia kufuatia uchunguzi unaoripotiwa kuhusu madai ya udanganyifu wa kimichezo, skendo ya uchunguzi wa vitendo vya ngono imeshika kasi nchini humo.
Haya yote yanafanyiwa uchunguzi ukiwamo wa kipolisi, ambapo ripoti mbalimbali zinadai huenda msimu huu ukamalizika huku ukiwa na amtukio mengi yanayochunguzwa na vyombo vya usalama kama ilivyokuwa 2023, ambapo kulikuwa na ukiukwaji wa matumizi ya kifedha yaliyosababisha Juventus kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya Ulaya kwa msimu mmoja.
Pia huenda ikakimbushia 2015, ambapo kulikuwa na kashfa ya uchunguzi mkubwa wa upangaji matokeo ya mechi uliohusisha michezo iliyopangwa katika ligi za chini na Lega Pro, huku 2011–12 kukiwa na kashfa ya upangaji matokeo maarufu kama Calcioscommesse ambayo ilisababisha watu wengi kukamatwa na timu kama Atalanta na Siena kupunguziwa pointi.
Mwaka 2006 ulikuwa na kashfa maarufu kama Calciopoli, ambapo ilihusisha klabu kadhaa kubwa kama Juventus, AC Milan, Lazio na Fiorentina.
Matokeo yake, Juventus ilishushwa daraja kutoka Serie A kwenda Serie B, huku klabu nyingine zikikumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo kupunguziwa alama.
Uchunguzi wa kashfa hizo haukuwaacha salama baadhi ya watu wakiwamo viongozi na wamiliki wa timu miongoni mwao wakiishia kupoteza nafasi zao katika klabu hizo na nyingine, huku viongozi wa Shirikisho la Soka Italia (FIGC) wakisombwa na maji.
Kwa sasa Rocchi ambaye ndiye anayehusika na kupanga waamuzi wa mechi za Ligi Kuu Italia (Serie A) kama sehemu ya majukumu yake, amelazimika kujiweka kando achunguzwe akidaiwa kukosea katika kanuni ambapo kuna waamuzi aliwaapingia mechi ambazo wanadaiwa kuwa na maslahi ya klabu husika, ambalo ni kinyume na kanuni.
Bosi huyo anachunguzwa kwa tuhuma za kushiriki katika udanganyifu msimu wa 2024/25, kwa mujibu wa taarifa za ofisi ya mwendesha mashtaka (AGI), na kikao cha awali cha mahakama kimepangwa kufanyika keshokutwa, Alhamisi, huku kujisimamisha kwake kuthibitishwa na Chama cha Waamuzi Italia (AIA).
Uchunguzi dhidi yake umeanzishwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Umma ya Milan na kwa mujibu wa taasisi hiyo, msimamizi wa VAR kwa ligi mbili za juu nchini Italia, Andrea Gervasoni, naye pia amejisimamisha baada ya kuwekwa chini ya uchunguzi.
Katika taarifa ya Chama cha Waamuzi wa Soka Italia (AIA), Rocchi (52), alikaririwa akisema: “Uamuzi huu mgumu na wa maumivu, ambao nimechukua kwa kushirikiana na familia yangu unalenga kuruhusu mchakato wa kisheria kuendelea bila vikwazo. Nina uhakika nitatoka katika hali hii nikiwa sina hatia na nikiwa imara zaidi kuliko hapo awali.”
Rocchi anatuhumiwa kumteua mwamuzi katika mechi mojawapo iliyohusisha Inter Milan aliyedaiwa kuwa mpenzi wa timu hiyo na katika tukio lingine, mwamuzi wa VAR hakuchukua hatua wakati mchezaji wa Inter alipompiga kiwiko mpinzani wake. Matukio yote mawili yako chini ya uchunguzi kwa sasa.
Nchini Italia, udanganyifu wa michezo ni kosa la jinai na linaweza kusababisha kifungo cha hadi miaka sita jela. Rocchi aliwahi kuwa mwamuzi wa Serie A kwa miaka 16 kati ya 2004 na 2020. Katika kazi yake, aliwahi pia kuchezesha fainali ya Coppa Italia 2016 pamoja na fainali ya Europa League 2019 ambapo Chelsea iliifunga Arsenal.
Kinachochunguzwa pia ni iwapo bosi huyo wa waamuzi alihusika katika matokeo ya mechi husika alizowapangia waamuzi wenye mapenzi na timu husika, kushinda au kushindwa.
Katika tukio jingine kuhusu kinachochunguzwa Rocchi anadaiwa kugonga mlango wa chumba cha waamuzi wa VAR wakati mechi ikiendelea kati ya Udinese dhidi ya Parma, na kuna video zinazoonyesha waamuzi wa VAR wakigeuka kana kwamba wanamuuliza Rocchi, ‘hii ni penalti?’ kisha kumwomba mwamuzi wa uwanjani aende kuangalia tukio hilo.
“Haya ndiyo madai yaliyopo kwa sasa, na yanahitaji kuthibitishwa kama yalivuruga ushindani na kufanya mechi kuwa siyo ya haki. Hapo ndipo tulipo kwa sasa,” anasema mwandishi maarufu za michezo wa Italia, Daniele Fisichella.
TUHUMA ZA NGONO
Kibongo bongo ishu binafsi za nje ya uwanja hazifuatiliwi sana, lakini kwa wenzetu pamoto! Skendo ya ngono inayohusisha zaidi ya mastaa 70 wakiwamo wanasoka imefikia patamu, ambapo tayari wameanza kufahamika na miongoni mwao wanaichezea AC Mila, Iter Milan, Juventus na Sassuolo.
Inawezekana wasibanwe sana, lakini kwa kuwa huduma hizo zinahusisha masuala ya ulipaji kodi, huenda wengi wakajikuta wakishtakiwa kwa sasa kinachoelezwa ni kwamba wengi hawakuwa wanalipa pale walipohudumiwa.






