UONGOZI wa klabu ya Simba, kupitia mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Swed Mkwabi, umeweka wazi kuwa maandalizi ya timu hiyo kuelekea fainali ya Kombe la Muungano hayana tofauti na yale waliyoyafanya katika hatua ya nusu fainali.
Mkwabi amesema benchi la ufundi chini ya kocha Steve Barker limeendelea na utaratibu ule ule wa maandalizi, wakiamini kuwa mbinu zilizowavusha kwenye hatua iliyopita zinaweza pia kuwapa mafanikio katika mchezo wa mwisho.
Amesisitiza kuwa kwa upande wa uongozi, wana imani kubwa na benchi la ufundi pamoja na wachezaji, hivyo hakuna sababu ya kubadili mfumo wa maandalizi kisa tu wanakwenda kucheza fainali.
Kwa mujibu wa Mkwabi, mchezo wa nusu fainali dhidi ya Mlandege SC umeonyesha dira sahihi ya timu, hivyo wanachofanya sasa ni kuendeleza kilekile walichokianza bila kufanya mabadiliko makubwa.
“Tuna imani na benchi la ufundi, sisi kama viongozi tupo nyuma yao. Hakuna maandalizi tofauti kwa sababu ya fainali, bali tunatumia yale yale tuliyotumia dhidi ya Mlandege SC kukabiliana na Yanga,” amesema Mkwabi.
Ameongeza kuwa lengo lao la kwanza lilikuwa kufika fainali, jambo ambalo tayari wamelitimiza, na sasa nguvu zao zote zimeelekezwa katika kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Kombe la Muungano.