Home Habari za michezo SIMBA WAPAMBANA NA KIVULI CHA VIPIGO VYA ZAMANI

SIMBA WAPAMBANA NA KIVULI CHA VIPIGO VYA ZAMANI

0

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema timu yao inaingia kwenye fainali ya Kombe la Muungano ikiwa na presha kubwa kutokana na matokeo ya nyuma dhidi ya wapinzani wao.

Ameeleza kuwa tofauti na wao, Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na hali ya kujiamini zaidi baada ya kuwafunga Simba mara tano katika michezo iliyopita, jambo linalowapa utulivu wa kisaikolojia kuelekea fainali hiyo.

Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo Simba watakuwa na kibarua kizito cha kujaribu kuizuia Yanga, mabingwa watetezi, ili kutwaa ubingwa huo.

“Presha ni kubwa kwetu kwa sababu tumekuwa tukipoteza mara kwa mara mbele ya mpinzani wetu. Tukipoteza tena, watu watajumlisha na matokeo ya nyuma, lakini tukishinda, wanaweza kusema ni bahati tu,” amesema Ahmed.

Aameongeza kuwa Yanga wataingia uwanjani wakiwa na ujasiri mkubwa kutokana na rekodi hiyo, huku Simba wao wakilazimika kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanalinda heshima ya klabu na kupata matokeo chanya.

Kuhusu waamuzi wa mchezo huo, Ahmed amesema ana imani watakaopangwa watasimamia sheria kwa haki na weledi, huku akisisitiza kuwa hawatarajii kuona makosa kama yaliyowahi kujitokeza hapo awali.