MENEJA wa kikosi cha Yanga, Walter Harrison amesema kuwa wamewasili Zanzibar wakiwa na lengo moja kuu la kutetea ubingwa wao wa Kombe la Muungano na kuendeleza rekodi nzuri waliyoijenga katika mashindano hayo
Harrison ameeleza kuwa maandalizi ya timu hiyo yamekuwa ya kiwango cha juu, huku benchi la ufundi likihakikisha wachezaji wanakuwa katika hali bora kimwili na kiakili kuelekea mchezo wa fainali unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya msimu uliopita yanawapa morali kubwa wachezaji, lakini pia yanawaweka katika presha ya kuhakikisha wanarudia ubora huo ili kulinda heshima ya klabu hiyo yenye historia kubwa ya ushindi.
“Yanga haitachukulia mchezo huo kirahisi licha ya kuwa mabingwa watetezi kwani wapinzani wetu wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri na nia ya kuvunja rekodi yao,” amesema.
Harrison amesema kuwa wachezaji wameelekezwa kucheza kwa nidhamu, kujituma na kutumia vizuri nafasi watakazopata ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya yatakayowawezesha kutwaa ubingwa huo kwa mara nyingine.
Amewataka mashabiki wa Yanga kuendelea kuwaunga mkono, akiamini kuwa sapoti yao ni chachu muhimu itakayowapa nguvu wachezaji kupambana hadi dakika ya mwisho na kufanikisha lengo lao la kutetea taji hilo.