Home Habari za michezo SIMEONE ATHIBITISHA ALVAREZ KUWANIWA NA ARSENAL, PSG NA BARCELONA

SIMEONE ATHIBITISHA ALVAREZ KUWANIWA NA ARSENAL, PSG NA BARCELONA

0

MADRID, HISPANIA: KOCHA wa Atletico Madrid, Diego Simeone amethibitisha kuwa Arsenal ni miongoni mwa klabu zinazomuwania mshambuliaji wao, Julian Alvarez.

Simeone alitoa kauli hiyo kabla ya mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo jana, Jumatano kati ya Atletico Madrid na Arsenal iliyochezwa jijini Madrid.

Mbali na Arsenal, klabu nyingine kubwa zinazomuwania Alvarez ni Paris Saint-Germain na Barcelona.

Simeone alisema: “Sipo ndani ya akili ya Julian Alvarez lakini ni kawaida kwa mchezaji wa kiwango chake kuhitajika na klabu kubwa kama Arsenal, PSG na Barcelona. Hiyo inaonyesha ubora wake.”

Alvarez, mwenye umri wa miaka 26, ameonyesha kiwango bora tangu ajiunge na Atletico akitokea Manchester City 2023 kwa ada ya Pauni 82 milioni. Tangu wakati huo, amefunga mabao 48 katika mechi 104.

Nyota huyo pia ni bingwa wa Kombe la Dunia 2022 akiwa na Argentina na ameendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Simeone.

Hata hivyo, Atletico Madrid hawana mpango wa kumuachia kirahisi nyota huyo kutokana na kuweka thamani yake kwa sasa kuwa ni Pauni 130milioni kiwango kinachoweza kuzikatisha tamaa klabu nyingi.

Inaelezwa kuwa, endapo Alvarez ataondoka, angependelea kujiunga na Barcelona, ingawa uwezekano wa uhamisho huo kufanyika katika dirisha lijalo la usajili bado ni mdogo.

Kwa sasa, mshambuliaji huyo ameweka kipaumbele chake katika kuisaidia Atletico Madrid kutwaa taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuelekeza nguvu zake kwenye Kombe la Dunia akiwa na Argentina.

Wakati huo huo, Arsenal wanapanga kufanya usajili mkubwa mwishoni mwa msimu, wakilenga kuongeza mshambuliaji, kiungo wa kati pamoja na beki wa pembeni ili kuimarisha kikosi chao.