DONETSK, UKRAINE: KLABU ya Shakhtar Donetsk inatarajiwa kupoteza kiasi cha Pauni 26 milioni kutokana na sakata la matumizi ya dawa haramu michezoni linalomkabili mchezaji wao wa zamani, Mykhailo Mudryk ambaye kwa sasa yupo Chelsea.
Mudryk alisajiliwa na Chelsea 2023 kwa ada inayofikia Pauni 88 milioni huku sehemu ya makubaliano ikijumuisha bonasi ya takribani Pauni 26 milioni inayotegemea mafanikio ya mchezaji na klabu hiyo.
Hata hivyo, kutokana na kusimamishwa kwake kwa muda kufuatia tuhuma za matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku, Shakhtar wanashindwa kunufaika na bonasi hizo kwa sasa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 hajacheza tangu Novemba 28, 2024, aliposhiriki mechi ya Europa Conference League na bado haijulikani ni lini atarejea uwanjani.
Mudryk alisimamishwa kwa muda Desemba 2024 baada ya kukutwa na sampuli yenye dawa iliyopigwa marufuku kabla ya kushtakiwa rasmi Juni 2025. Inaelezwa kuwa dawa hiyo ni meldonium.
Mkurugenzi mkuu wa Shakhtar, Sergei Palkin alisema: “Tuna bonasi ya pauni 26 milioni kwenye mkataba wake. Kama hachezi au Chelsea hawapati matokeo mazuri, tunapoteza fedha hizo. Hii ni hasara kubwa kwetu.”
Aliongeza kuwa bado wana imani Mudryk atarejea uwanjani: “Namfahamu kama mchezaji na kama mtu. Ninaamini atarudi na kuanza kucheza tena.”
Inaelezwa kuwa mkataba wa Mudryk unaoisha mwaka 2031 pia unajumuisha bonasi za kushinda Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya na malipo binafsi kulingana na kiwango chake.
Endapo atapatikana na hatia, Mudryk anaweza kufungiwa hadi miaka minne nje ya soka. Hata hivyo, hadi sasa hakuna tarehe rasmi ya uamuzi wa kesi yake.
Rais wa World Anti-Doping Agency, Witold Banka, alisema bado wanasubiri uamuzi wa nidhamu kutoka kwa FA kabla ya kuchukua hatua zaidi.
Kwa upande wake, Mudryk amekuwa akikanusha tuhuma hizo kwa kusema hajawahi kutumia dawa zilizopigwa marufuku kwa makusudi.