Home Habari za michezo JULIO AICHIMBA MKWARA MBEYA CITY

JULIO AICHIMBA MKWARA MBEYA CITY

0

KOCHA wa Mashujaa, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameichimbia mkwara mzito Mbeya City, akisisitiza kikosi chake kimejipanga kikamilifu kuondoka na pointi tatu dhidi yao.

Kauli ya Julio imekuja kipindi hiki ambacho anakiandaa kikosi chake kwenda Mbeya kukabiliana na Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo.

Akizungumzia maandalizi kuelekea pambano hilo, Julio alisema wanaboresha safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha wanatumia vyema nafasi wanazozitengeneza.

“Tumejiandaa vizuri kwa mchezo huu, tumefanya mazoezi ya kutosha ya kutengeneza nafasi na kufunga. Lengo letu ni moja tu, kupata pointi tatu,” alisema Julio.

Aliongeza, ana imani kubwa na washambuliaji wake, akieleza kuwa muda umefika kwao kuonyesha makali yao kuanzia kwenye mchezo huo dhidi ya Mbeya City.

“Ninaamini washambuliaji wangu wataanza kufanya kazi yao ipasavyo kwenye mechi hii. Tunahitaji mabao na nina uhakika watafunga,” alisema.

Mbeya City ina kibarua kizito cha kujinusuru kutoshuka daraja, huku ikiwa na mechi 11 mkononi zitakazoamua hatima hiyo, huku ikishika nafasi ya 14 kwenye msimamo ikiwa na pointi 17.

Mashujaa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imeshinda mechi nne, sare tisa na kupoteza sita, ikifikisha jumla ya pointi 21.

Julio ambaye amewahi kuinoa Mwadui, Coastal Union, Simba na Taifa Stars, alianza kazi ya kukiongoza kikosi cha Mashujaa Februari 13, 2026 baada ya kuondoka Salum Mayanga na mechi ya kwanza ya ligi alishinda 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha zikafuatia sare nne mfululizo dhidi ya Fountain Gate (1-1), Azam (0-0), Pamba Jiji (0-0) na Singida Black Stars (1-1), hajapoteza.