Home Habari za michezo DUKE ABUYA AWAIBUA WAKONGWE

DUKE ABUYA AWAIBUA WAKONGWE

0

INGAWA jina la kiungo wa Yanga, Duke Abuya haliimbwi mara kwa mara na mashabiki, lakini kuna mafundi wa mpira wa miguu wakongwe wameona anachokifanya ni kikubwa na kina matokeo chanya katika klabu hiyo.

Kiungo mkabaji aliyewahi kuzichezea Simba, Yanga, Azam FC na Taifa Stars, Athuman Idd Chuji, alisema wakati mwingine kutajwa kila kona inategemea na nyota ya mchezaji lakini haimanishi asiyetajwa hafanyi kazi kubwa, akimtolea mfano Abuya jinsi anavyosaidiana na mabeki kulinda usalama wa kutokufungwa.

Chuji alisema Abuya ni mchezaji anayenyumbulika katika majukumu yake, kuna wakati anaisaidia timu kushambulia na kutengeneza nafasi ya wengine kufunga mabao.

“Kwangu binafsi Abuya ni kati ya viungo bora wa chini katika Ligi ya Tanzania, ana umakini wa kuokoa hatari bila kusababisha faulo, mtulivu wa maamuzi, anajua ni muda gani wa kutoka kwenda kushambulia bila kuacha pengo nyuma,” alisema Chuji na kuongeza;

“Mtu anayejua mpira anaelewa ninachokizungumza, binafsi nampongeza na aendelee kupambana haijalishi jina lake halina kelele nyingi kwa watu wa familia ya soka, lakini wanaojua mpira wanafurahishwa na anachokifanya.”

Katika Ligi Kuu inayoendelea msimu huu, Abuya amefunga bao moja na asisti tano, wakati 2024-2025 alikuwa na mabao matatu, asisti mbili na 2023-2024 mabao yalikuwa manne na asisti tatu.

Jambo ambalo staa wa zamani wa Simba, Yanga, Mtibwa na Taifa Stars, Mohamed Banka alisema kuhusu Abuya ni: “Ni kiungo mzuri, anafanya kazi yake kwa nidhamu ya hali ya juu na utulivu, haijalishi timu inakuwa katika wakati mgumu ama mzuri.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa klabu hiyo na Stars, Oscar Joshua ingawa alicheza beki, lakini alimzungumzia Abuya: “Kiungo wa chini wakifanya kazi yao vizuri inakuwa rahisi kwa beki kazi yake kuwa nyepesi, jamaa anajua na ana kipaji kikubwa.”