Home Habari za michezo DUKE, DAMARO, MAX WABEBA NDOTO ZA YANGA FAINALI

DUKE, DAMARO, MAX WABEBA NDOTO ZA YANGA FAINALI

0

MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi chao kimejipanga kikamilifu kwa fainali ya Kombe la Muungano kufuatia kauli ya Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ambayo imeongeza hamasa ndani ya timu hiyo.

Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani leo kuwakaribisha watani wao wa jadi Simba katika fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, huku kila upande ukihitaji ushindi ili kubeba taji hilo muhimu.

Kamwe amesema kauli ya Ahmed Ally, aliyetamani Yanga ifike fainali ili wakutane, imepokelewa kama dharau kwa wachezaji wao, jambo ambalo limewapa motisha ya ziada kupambana kwa nguvu zote.

“Ile kauli kwetu imeonekana kama kudharau uwezo wa wachezaji wetu. Ndiyo maana katika maandalizi ya mechi hii, tumewapa jukumu kubwa wachezaji wetu kupambana hadi mwisho,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa nyota wao muhimu, Duke Abuya, Mohammed Damaro na Max Nzengeli, wamepewa wajibu maalum wa kuhakikisha wanapambana kwa moyo wote uwanjani, wakilenga kulinda heshima ya klabu hiyo.

“Tumewaambia wazi, kama ni kupigania heshima ya Yanga, basi wapambane bila kuacha chochote uwanjani. Max alichoonyesha dhidi ya Azam FC tunataka akiongeze mara nne katika fainali hii,” ameongeza.

Kamwe amesisitiza kuwa hawapo tayari kurudia makosa ya mchezo wa Kariakoo Derby ya mzunguko wa kwanza uliochezwa katika dimba hilo, ambapo walilazimishwa sare ya bila kufungana. Amesema safari hii wanahitaji ushindi ili kuondoka na taji.