WAKATI Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga akiweka wazi mkakati wa kuirejesha timu hiyo kwenye ubora wake, kiungo mshambuliaji Hassan Dilunga ameongeza hamasa kwa kutangaza vita kali katika mechi zilizobaki msimu huu.
Mbeya City, ambayo imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu, imekuwa ikisota kupata matokeo chanya licha ya jitihada za uongozi na mashabiki kuendelea kuiunga mkono ili kuhakikisha inabaki salama na kuepuka kushuka daraja.
Hivi sasa timu hiyo inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 17, na inajiandaa kwa mchezo muhimu dhidi ya Mashujaa utakaochezwa Aprili 30 mwaka huu.
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Kocha Mayanga tangu ajiunge na kikosi hicho kuchukua mikoba ya Mecky Maxime.
Akizungumzia hali ya timu, Dilunga amekiri kuwepo kwa presha kubwa kwa wachezaji na mashabiki kutokana na mwenendo wa matokeo, lakini amesisitiza kuwa bado wana nafasi ya kupambana na kubadili hali ilivyo.
Amesema katika mechi 11 zilizobaki, lengo lao ni kushinda kila mchezo kwa dakika 90 ili kujikusanyia pointi muhimu, akibainisha kuwa tofauti ya pointi kati yao na timu zilizo juu si kubwa kiasi cha kuwakatisha tamaa.
“Tunajua mashabiki hawajafurahishwa na matokeo yetu, lakini tunawaomba waendelee kuwa na imani nasi. Tuko tayari kupambana kuhakikisha Mbeya City inabaki Ligi Kuu,” amesema Dilunga.
Ameongeza kuwa kwa sasa wako katika nafasi ya mchujo (play-off), lakini wanaamini wakiongeza juhudi wanaweza kupanda zaidi kwenye msimamo, kwani ushindani uliopo bado unaruhusu mabadiliko.
Dilunga, aliyewahi kuichezea Simba na JKT Tanzania, amesema ligi imekuwa ngumu zaidi kadri inavyoelekea ukingoni, hivyo amewataka wachezaji wenzake kuongeza ari, umoja na kujiamini ili kufanikisha malengo ya timu.