Hata hivyo, Rommy3D hakupuuza uwezo wa watani wao wa jadi Simba akisema walionyesha kiwango kizuri.
Licha ya unazi wake kwa Yanga, amekiri kuvutiwa na vipaji vya baadhi ya wachezaji wa Msimbazi, akiwataja beki mwenye mapafu ya mbwa, Shomari Kapombe, pamoja na kiungo mshambuliaji Libase Gueye.
Rommy hakusita pia kumtaja beki wa zamani wa timu hiyo, Enock Inonga, kama mmoja wa wachezaji waliomvutia zaidi licha ya kuwa tayari ameshatimka kikosini hapo.
Hatua hiyo ya Rommy3D imepokelewa kwa hisia chanya mtandaoni, ambapo wadau wengi wa soka wamesifu uwezo wake wa kutofautisha ushabiki na utaalamu wa soka.
Mashabiki wameitaja kauli yake kama ishara ya upendo na weledi, ikionyesha kuwa michezo ni chombo cha kuunganisha watu na kwamba inawezekana kabisa kuthamini kazi nzuri ya mchezaji hata kama anavaa jezi ya mpinzani wako.