Home Habari za michezo ARSENAL VS ATLETICO MADRID, VITA YA FAINALI YAWAKA EMIRATES

ARSENAL VS ATLETICO MADRID, VITA YA FAINALI YAWAKA EMIRATES

0

LONDON, ENGLAND: LEO ndiyo leo pale Emirates. Mashabiki wa Arsenal na Atletico Madrid kwa sasa roho mkononi wakisubiri hatma yao ya kwenda fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baada ya sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Hispania, vita ya mwisho ni leo jijini London na Arsenal itaikaribisha Atletico Madrid katika mechi ya nusu fainali.

Kwa Arsenal, inataka kuandika ukurasa mpya baada ya miaka 20 ya kusubiri kurejea fainali ya michuano hiyo mikubwa Ulaya.

Kikosi hicho cha Mikel Arteta kitaingia katika mechi hii kikiwa hakijapoteza hata mechi moja ya Ligi ya Mabingwa (ushindi 10, sare 3), huku safu yao ya ulinzi ikiwa haijaruhusu bao katika mechi nane.

Huu ni msimu ambao mashabiki wa Arsenal wameusubiri kwa hamu msimu wa kuamini tena kwenye maajabu. Dalili za mafanikio zimeonekana wazi mwishoni mwa wiki baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fulham, matokeo yaliyowapa nafasi nzuri kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England. Lakini zaidi ya matokeo hayo, kilichowavutia wengi ni namna Arsenal walivyocheza kwa uhuru, kasi na ubunifu, hivyo wanaingia kwenye mechi hii wakiwa katika kiwango bora kabisa.

Upande mwingine, Uwanja wa Emirates umekuwa tishio kwa wapinzani. Arsenal wamepoteza mechi moja kati ya 24 walizocheza nyumbani katika michuano ya Ulaya, wakishinda 17 na kutoa sare sita.

Msimu huu pekee, wameshinda michezo mitano kati ya sita ya nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa, wakionyesha wazi kuwa wanajua namna ya kutumia faida ya uwanja wao.

Hata hivyo, Atletico Madrid sio timu ya kuchukulia poa. Wakiwa chini ya kocha wao mwenye uzoefu mkubwa Diego Simeone, wamejijengea sifa ya kupambana, hasa katika michezo mikubwa ya Ulaya.

Ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Valencia mwishoni mwa wiki, licha ya kufanya mabadiliko makubwa kikosini, umeonyesha kuwa wana kikosi kipana na uwezo wa kuhimili presha.

Atletico wanaingia kwenye mechi hii wakijua wazi kuwa sare haitoshi wanahitaji ushindi. Historia inaonyesha wanaweza kufanya hivyo, kwani wameshinda michezo sita kati ya saba ya nusu fainali za Ulaya walizocheza, ikiwemo dhidi ya Arsenal 2018 kwenye Europa League.

Lakini changamoto kubwa kwao ipo kwenye rekodi mbaya ya ugenini. Katika michezo yao 10 ya mwisho ugenini, wameshinda mitatu huku wakipoteza sita. Zaidi ya hapo, wamepoteza mechi tatu za ugenini za Ligi ya Mabingwa msimu huu zote dhidi ya timu za England.

Historia ya mechi kati yao pia inaipa nguvu Arsenal katika uwanja huu waliwahi kuichapa Atletico mabao 4-0 na kwa ujumla hawajapoteza katika michezo tisa ya karibuni dhidi ya timu za Hispania.

Kwa upande mwingine, Atletico wamepoteza mechi sita kati ya saba walizocheza nchini England takwimu ambazo zinaweza kuathiri morali yao kabla ya pambano hili kubwa.

MBINU NA VITA YA UFUNDI

Kiufundi huu ni mchezo wa mbinu kati ya falsafa mbili tofauti, Arsenal wanapendelea mpira wa kumiliki, wakitumia mfumo unaobadilika kati ya 4-3-3 na 3-2-5 wanaposhambulia. Hapa, mabeki wa pembeni hupanda juu, huku viungo wakijaza katikati ili kutengeneza nafasi na kuisukuma Atletico nyuma.

Kiungo kama Martin Odegaard anakuwa kiungo muhimu katika kuunganisha safu ya kati na ushambuliaji, wakati Bukayo Saka akitumia kasi na ubunifu wake pembeni kuvunja ngome ya wapinzani.

Arsenal pia hutegemea kukabia juu wanapopoteza mpira ili kuwanyima wapinzani muda wa kupanga mashambulizi.

Kwa upande wa Atletico, Simeone anajulikana kwa mfumo wake wa 4-4-2 wenye nidhamu kali ya kujilinda. Timu yake hupunguza nafasi kwa kucheza kwa mistari miwili iliyokaribiana, wakisubiri nafasi ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza (counter-attacks).

Hapa ndipo hatari yao ilipo kwa kasi ya Alvarez na ubunifu wa Antoine Griezmann, Atletico wanaweza kuadhibu makosa madogo ya Arsenal. Pia mipira ya adhabu au kuona inaweza kuwa silaha muhimu kwao.

HALI YA VIKOSI

Kwa upande wa Arsenal, kuna matumaini makubwa ya kurejea kwa Martin Odegaard na Kai Havertz lakini Jurrien Timber na Mikel Merino wataendelea kukosekana kwenye kikosi hicho.

Kwa Atletico, Alvarez anatajwa kuwa fiti licha ya hofu ya awali ya majeraha na anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Alvarez aliandika historia baada ya kuvunja rekodi ya Lionel Messi, kwa kuwa Muargentina aliyefikisha mabao 25 ya Ligi ya Mabingwa kwa haraka zaidi akifanya hivyo ndani ya michezo 41, wakati Messi alihitaji michezo 42 kufikia idadi hiyo.

Wachezaji kama Giuliano Simeone, Marcos Llorente, Alexander Sorloth na David Hancko walipumzishwa wikiendi iliyopita lakini Jose Gimenez bado yuko kwenye hatihati huku Pablo Barrios na Nico Gonzalez wakikosekana.