WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC, wametangaza rasmi kuhama kutoka Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni na kuhamishia michezo yao ya nyumbani kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, huku sababu ya kufanya hivyo ikibainika.
Uamuzi huo umetangazwa leo Alhamisi Mei 7, 2026, ikiwa ni siku moja tu baada ya kocha mkuu wa Simba, Steve Barker kulalamikia ubora wa eneo la kuchezea la Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kufuatia ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Barker alisema mazingira ya uwanja huo yamekuwa yakiiathiri timu kucheza soka lao la kawaida, akieleza kuwa wanalazimika kutumia nguvu kubwa tofauti na mfumo wao wa pasi na kasi waliouzoea.
Hii sio mara ya kwanza kwa kocha huyo kulizungumzia suala hilo, kwani hata baada ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2, aliweka wazi kutoridhishwa kwake na eneo la kuchezea akidai lilikuwa changamoto kubwa kwa wachezaji.
Mabadiliko hayo sasa yataifanya Simba kuutumia Uwanja wa KMC Complex katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa Jumapili, Mei 10, 2026. Hivyo kuwa timu ya tatu kutumia uwanja huo kwa michezo yake ya nyumbani, awali ulikuwa ukitumiwa na wenyewe, KMC pamoja na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga.
Awali Simba ilikuwa ikitumia uwanja huo kwa mechi zake za nyumbani kabla ya kuhamia Isamuhyo na kuwaacha watani zao, Yanga na KMC.
Baada ya kumalizana na Prisons, Simba itasafiri hadi Kigoma kuikabili Mashujaa FC kabla ya kuelekea Tanga kuivaa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Kwa sasa Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 46, huku Yanga ikiongoza kwa pointi 51 baada ya timu hizo kutoka sare katika dabi iliyopita.
Licha ya pengo hilo la pointi tano, Simba bado inaendelea kuwa kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi ilioukosa kwa misimu minne mfululizo.