UONGOZI wa Yanga SC umeweka wazi sababu za kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pedro Gonçalves, ukieleza kuwa maamuzi hayo hayakutokana na matokeo ya uwanjani pekee bali tathmini ya kina ya mwenendo mzima wa kikosi hicho.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe amesema viongozi wa klabu walifanya tathmini kubwa iliyohusisha kiwango cha uchezaji, mfumo wa timu pamoja na namna ambavyo ushindi ulikuwa ukipatikana ndani ya uwanja.
Pedro alitangaziwa kuachana na Yanga jana mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya KMC ambao mabingwa hao walishinda bao 1-0, huku sehemu ya mashabiki wakionyesha kutoridhishwa na kiwango cha timu licha ya kupata matokeo chanya.
Kamwe amesema Yanga haiangalii pointi pekee katika kufanya maamuzi, bali huzingatia pia ubora wa soka linalochezwa na taswira ya timu kwa ujumla.
“Uongozi ulifanya tathmini sio matokeo peke yake, wala idadi ya pointi au mabao ya kufunga na kufungwa,” amesema Kamwe.
Amefafanua kuwa klabu hiyo ina malengo makubwa yanayoendana na hadhi yake, hivyo ni lazima timu ionekane kucheza kwa kiwango kinachowaridhisha viongozi na mashabiki wake.
“Tunashinda lakini tunashindaje? Timu kama Yanga inakusanya vitu vingi. Kuna uongozi wa timu, kiwango cha timu na namna ya ushindi wenyewe,” amesema.
Kwa mujibu wa Kamwe, tathmini hiyo ilibaini kuwa kiwango cha timu hakikuwa katika kiwango kinachotarajiwa, jambo lililoonekana wazi kwa mashabiki wengi waliokuwa wakifuatilia mechi za timu hiyo hivi karibuni.
“Tumefanya tathmini na kugundua timu haina mwenendo mzuri. Kila Mwanayanga aliyekuwa akiangalia timu aliona hatuchezi katika kiwango kinachotarajiwa,” amesema.
Kamwe pia alizungumza kwa utani akisema hata ushindi wa Yanga umeendelea kuwapa presha wapinzani wao wa jadi, akidai furaha yao imepungua katika siku za karibuni.
Kwa sasa benchi la ufundi la Yanga linaongozwa kwa muda na Patrick Mabedi pamoja na Abdihamid Moallin wakisaidiana na Mathew Silva katika majukumu ya kiufundi huku klabu ikiendelea kutafuta mwelekeo mpya kuelekea mwisho wa msimu.
Uongozi wa klabu hiyo umeeleza kuwa maamuzi yote yaliyofanyika yana lengo la kuhakikisha Yanga inafikia malengo yake makubwa ya msimu huu.
“Haijalishi tuna makocha wangapi, mwisho wa msimu tunapata nini ndiyo jambo muhimu kwetu,” amesema Kamwe.
Wakati huohuo, Yanga inaendelea na maandalizi ya mchezo wake ujao dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Jumamosi, huku mashabiki wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao.