KIUNGO mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama amesema bao lake la kuvutia alilofunga kwenye dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC limekuwa gumzo kubwa kiasi cha kushindwa kuamini namna lilivyopokelewa na mashabiki wa soka duniani.
Chama amesema hakutarajia kama bao hilo lingezua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari, akieleza kuwa lilikuwa ni tukio lililotokea kwa ubunifu na kujiamini akiwa ndani ya uwanja.
Akizungumza kupitia mazungumzo maalumu yaliyowekwa wazi mtandaoni, nyota huyo alisema bao hilo ni miongoni mwa mabao bora kabisa kuwahi kufunga katika maisha yake ya soka kutokana na ugumu wake pamoja na presha ya mchezo wa dabi.
“Lilikuwa bao kubwa na kitu ambacho hata mimi sikukitarajia. Natamani lipate heshima inayostahili,” alisema Chama akizungumzia bao hilo lililoacha gumzo kwa mashabiki wengi wa soka Afrika Mashariki.
Katika mazungumzo hayo, Chama pia alikiri kuwa huenda bao hilo likawa bora zaidi kuwahi kufunga tangu aanze kucheza soka la ushindani, jambo lililoongeza mjadala mkubwa kwa mashabiki wa Simba na wapenda soka kwa ujumla.
Bao hilo limeendelea kusambazwa kwa kasi kwenye majukwaa mbalimbali ya kijamii huku wengi wakilitaja kama moja ya mabao mazuri zaidi kuwahi kufungwa kwenye dabi ya Kariakoo katika miaka ya karibuni.
Mashabiki wa Simba wameendelea kumpongeza kiungo huyo kwa ubunifu wake mkubwa huku wakiamini uwezo wake bado una mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho kinachowania mataji msimu huu.