KIUNGO mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama amesema wao kama wachezaji wataendelea kupambana hadi dakika ya mwisho kuhakikisha timu hiyo inapata ushindi katika kila mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba jana iliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, huku Chama akiwa shujaa wa mchezo huo baada ya kufunga bao pekee la ushindi.
Baada ya mchezo huo, Chama amesema ushindi huo haukuwa rahisi kutokana na uchovu uliotokana na ratiba ngumu ya mechi walizokuwa wakicheza katika siku za karibuni.
Nyota huyo amesema walikuwa na mpango wa kupata bao la mapema ili kuupa utulivu mchezo na kuwasaidia kuutawala kwa urahisi zaidi.
“Mchezo haukuwa mwepesi kwetu, hasa kipindi cha kwanza. Tulihitaji kupata bao mapema ili kutupa nafasi ya kuutawala mchezo kwa sababu tulitoka kucheza Jumapili, hivyo kulikuwa na uchovu wa ratiba,” amesema Chama.
Amesema baada ya kushindwa kupata bao ndani ya dakika 45 za kwanza, walirejea kipindi cha pili wakiwa na ari mpya kufuatia maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi.
“Tuliporudi kutoka mapumziko, kocha alitusisitiza kuongeza nguvu na kupambana zaidi ili kuhakikisha tunapata bao la ushindi,” amesema.
Mbali na kuipa Simba alama tatu muhimu, Chama pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa wa timu nzima.
“Tuzo hii si yangu peke yangu, ni ya timu nzima kwa sababu kila mmoja alipambana kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Chama.