Home Habari za michezo VITA YA UBINGWA YAPAMBA MOTO, SIMBA YAKATAA KUKATA TAMAA

VITA YA UBINGWA YAPAMBA MOTO, SIMBA YAKATAA KUKATA TAMAA

0

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema timu hiyo itaendelea kupambana kuhakikisha inashinda michezo yote iliyosalia katika kampeni yao ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Ahmed amesema Simba tayari imeanza vizuri kampeni hiyo baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya JKT Tanzania, huku akisisitiza kuwa malengo yao kwa sasa ni kuhakikisha wanapata ushindi katika kila mchezo uliopo mbele yao.

“Kama ilivyo kampeni yetu tuliyotangaza, katika michezo 10 tuliyokuwa tumesalia nayo sasa imebaki tisa na tunahitaji kushinda yote,” amesema Ahmed huku akieleza kuwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi wamejipanga kuhakikisha wanatimiza azma hiyo.

Ameongeza kuwa licha ya tofauti ya alama tano iliyopo kati yao na vinara wa ligi, Simba haitakiwi kukata tamaa kwani jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanavuna pointi tatu katika kila mchezo watakaocheza kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu.

Ahmed amesema ushindi walioupata dhidi ya JKT Tanzania ulikuwa muhimu kwa sababu ulikuja dhidi ya timu ngumu iliyowapa upinzani mkubwa, jambo ambalo limeongeza morali ndani ya kikosi hicho kuelekea michezo ijayo.

Baada ya mchezo huo, amesema Simba sasa imerejea kambini kuanza maandalizi ya mchezo wao ujao dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa Mei 10, akibainisha kuwa licha ya wapinzani wao kuwa katika kipindi kigumu, mchezo huo hautakuwa rahisi hata kidogo.

“Unaweza kuona wana hali mbaya na wamepoteza mechi nyingi, lakini timu zinazopigania kubaki ligi kuu huwa hatari sana kwa sababu kila mchezo kwao ni wa maisha au kifo. Hawatakubali kufungwa kirahisi, lakini sisi tunaingia uwanjani kupambana kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu,” amesema Ahmed.