Siku chache baada ya kutimuliwa ndani ya Yanga SC, aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pedro Gonçalves, amevunja ukimya kwa ujumbe mrefu wa kuaga uliogusa hisia za mashabiki wa klabu hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Pedro amesema kuondoka kwake ni “mwisho bila hitimisho,” kauli iliyoibua mjadala mkubwa miongoni mwa Wana Yanga.
Kocha huyo raia wa Ureno amesema anaondoka akiwa na kumbukumbu nyingi zisizofutika pamoja na uzoefu mkubwa wa kazi alioupata Tanzania. Pedro alikumbusha namna alivyoikuta Yanga mwanzoni mwa safari yake, wakati timu ikiwa nyuma kwa pointi mbili dhidi ya watani wao wa jadi, lakini akaondoka akiwa ameiacha kileleni mwa msimamo wa ligi.
“Ninaondoka nikiwaacha pointi tano kileleni, nafasi ya kwanza, timu yenye mabao mengi, iliyoruhusu mabao machache, na timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote wa ligi msimu huu,” ameandika Pedro katika sehemu ya ujumbe wake wa kuaga.
Mbali na hilo, Pedro hakusita kujivunia mafanikio aliyoyapata ndani ya kikosi hicho. Katika mechi 35 za mashindano yote aliyoiongoza Yanga, aliibuka na ushindi mara 25 huku akipoteza michezo mitatu pekee.
Vipigo hivyo viwili vilikuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na FAR Rabat ugenini, huku kingine kikitokea kwenye fainali ya Muungano Cup baada ya dakika 120 za mchezo.
Chini ya Pedro, Yanga pia ilifanikiwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kusonga mbele katika hatua tatu za Kombe la FA pamoja na kutwaa Kombe la Mapinduzi. Licha ya kuondolewa kwake kabla ya mwisho wa msimu, kocha huyo anaamini msingi aliouweka utaisaidia timu kutwaa ubingwa wa ligi iwapo nidhamu itaendelea kudumishwa.
Pedro alihitimisha kwa kuwashukuru viongozi, wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wote wa Yanga kwa ushirikiano waliompa tangu alipowasili Tanzania.
Kuondoka kwake kumeacha gumzo kubwa Jangwani, hasa kutokana na takwimu nzuri alizoacha nyuma. Wengi wamebaki wakijiuliza kama kweli ulikuwa wakati sahihi wa kuachana naye, huku kauli yake ya “mwisho bila hitimisho” ikiendelea kubeba uzito mkubwa kwa mashabiki wa Wananchi.