Home Habari za michezo VIJIMAMBO KUMI WABABE, VIBONDE MZIGONI EPL

VIJIMAMBO KUMI WABABE, VIBONDE MZIGONI EPL

0

LONDON, ENGLAND: JANA, Ijumaa, mechi nnne katika ligi nne kubwa Ulaya zilipigwa kuelekea wikiendi ambayo itakuwa na pilikapilika nyingi katika ligi tano zote bora Ulaya, ikiwa ni mechi za mwisho mwisho kabla ya kumalizika kwa msimu huu.

Tayari mabingwa wawili katika ligi hizo wameshapatikana na Bayern Munich imeshabeba ubingwa wa Ujerumani (Bundesliga) huku Inter Milan ikichukua ule wa Italia (Seri A) na sasa vita imebakia England (EPL), Ufaransa (Ligue 1) na Hispania (LaLiga).

Sikia! Katika Ligi Kuu England inayoendelea pia kuanzia leo hadi Jumatatu kabla ya kusikilizia kwa siku moja hapo kati wiki ijayo, kuna mitego kama 10 hivi inayoangaliwa katika mechi za wikiendi hii, na hii ndiyo yenyewe:

1. SLOT VS CHELSEA

Kocha Arne Slot wa Liverpool anataka kuitumia mechi dhidi ya Chelsea ili kukata tiketi ya mashindano ya Ulaya msimu ujao. Liverpool wameondoa tatizo moja walilojitengenezea wenyewe baada ya kuwasikiliza mashabiki wao na kufuta mpango wa kuongeza bei za tiketi kwa misimu mitatu ijayo. Sasa macho yanaelekezwa katika kuhakikisha wanapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Liverpool watajihakikishia kumaliza ndani ya tano bora iwapo wataifunga Chelsea, huku Bournemouth wakishindwa kuifumua Fulham. Slot hawezi kutamani mpinzani bora zaidi kuliko Chelsea ya sasa, timu iliyojaa migogoro na wachezaji wanaocheza wanapotaka tu. Chelsea wamepoteza mechi saba mfululizo za ligi mara moja tu katika historia, mwaka 1952. Wanaweza kurudia rekodi hiyo mbaya wakifungwa Anfield. Wamefungwa kwa tofauti ya mabao matatu katika mechi mbili zilizopita ugenini na matatu au zaidi katika mechi nne kati ya tano za mwisho za ligi.

2. BRIGHTON NA HURZELER

Kocha Fabian Hurzeler amepewa kandarasi mpya ya miaka mitatu hadi 2029 baada ya kufufua matumaini ya Brighton kucheza Ulaya. Mustakabali wake ulikuwa shakani Februari baada ya mwanzo mbaya wa mwaka, lakini ushindi mara sita katika mechi tisa umeifanya Brighton kuwa karibu tena na nafasi za Ulaya. Ushindi dhidi ya Wolves ni muhimu kabla ya safari ya kuifuata Leeds United na mchezo dhidi ya Manchester United siku ya mwisho wa msimu.

3. SILVA WA FULHAM

Kocha Andoni Iraola tayari ameamua kuondoka Bournemouth mwishoni mwa msimu, lakini hali bado haijawa wazi kwa Marco Silva wa Fulham. Silva pia kandarasi yake inaelekea mwisho na anawaza kama huu ndio wakati sahihi wa kuondoka na aliijenga Fulham miaka mitano, akiipandisha kutoka Championship hadi kuwa timu imara Ligi Kuu England. Fulham ina nafasi nzuri ya kucheza Ulaya ikishinda dhidi ya Bournemouth, lakini Silva anaweza kuhisi amefika kikomo na kutaka changamoto mpya.

4. MAN UNITED VS SUNDERLAND

Michael Carrick anajua vizuri uwezo wa Regis Le Bris baada ya Sunderland kuwafunga Middlesbrough mara mbili msimu uliopita. Manchester United hawawezi kuidharau Sunderland, timu iliyopanda daraja, lakini bado ina ndoto za kucheza Ulaya. Winga wa Man United, Amad Diallo anatarajia kurejea Sunderland ambako aliwahi kung’ara akiwapo kwa mkopo.

“Tony Mowbray alikuwa kama baba kwangu. Naipenda Sunderland na ninafurahia kuona wanafanya vizuri,” alisema Amad.

5. JOHN STONES VS BRENTFORD

Je, huu ni mchezo wa John Stones? Manchester City wakitaka kutetea ubingwa lazima wafunge mabao mengi, lakini matatizo yapo zaidi katika safu yao ya ulinzi.

Abdukodir Khusanov na Marc Guehi walikuwa na wakati mgumu dhidi ya Everton, hivyo kocha Pep Guardiola anaweza kumrudisha John Stones kutokana na utulivu wake akiwa na mpira. Stones ana miezi chini ya miwili kubaki Man City na hataki kumalizia muda wake benchi. Atataka kusaidia katika mbio za ubingwa huku fainali ya FA ikikaribia.

6. AMDOUNI KUIPA FURAHA BURNLEY?

Licha ya kwamba tayari Burnley imeshashuka daraja, lakini Zeki Amdouni alirejea uwanjani baada ya kukaa nje siku 291 kutokana na majeraha ya goti. Katika msimu mbaya wa Burnley, kurejea kwake ni habari njema kwa mashabiki. Kocha wa muda, Mike Jackson, anaweza kutumia mchezo dhidi ya Aston Villa kumpa nafasi ya kuonyesha uwezo na kuwapa matumaini mashabiki waliokata tamaa mapema.

7. CRYSTAL PALACE KUAMUA BINGWA?

Licha ya Crystal Palace kutokuwa salama kabisa dhidi ya kushuka daraja, kocha Oliver Glasner anaweza kupumzisha baadhi ya nyota wake dhidi ya Everton kutokana na uchovu wa Conference League. Lakini, mchezo dhidi ya Manchester City wiki ijayo unaweza kuwa muhimu zaidi katika mbio za ubingwa. Ikiwa Palace bado watahitaji pointi kujinusuru, wanaweza kucheza kwa nguvu zote dhidi ya City. Baadaye watakutana na Brentford na Arsenal, hivyo wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuamua bingwa wa Ligi Kuu.

8. ELANGA KUREJEA NYUMBANI

Anthony Elanga anatarajiwa kurejea sehemu anayojulikana zaidi Nottingham Forest kabla hajatimkia alipo sana. kocha wake, Eddie Howe anataraji kubakia Newcastle United baada ya msimu kumalizika, hivyo anatumia mechi zilizobaki kuamua nani ataendelea naye. Elanga, Nick Woltemade na Anthony Gordon walibaki benchi katika ushindi dhidi ya Brighton.

Lakini, Elanga kwa sasa anarudi City Ground ambako aliwahi kung’ara akiwa Nottingham Forest. Mazingira anayoyafahamu yanaweza kumsaidia kuonyesha ubora wake tena dhidi ya timu inayomjua vizuri.

9. PABLO FELIPE VS ARSENAL

Supastaa wa West Ham United, Pablo Felipe anatakiwa kuonyesha uwezo mkubwa dhidi ya Arsenal katika mechi yenye uamuzi kuhusu hatima ya timu zote mbili.

Felipe amekuwa akijituma tangu ajiunge na West Ham kutoka Gil Vicente, Januari, mwaka huu, lakini bado hajafunga bao. West Ham walimnunua kwa Pauni 18.3 milioni na bado wanaamini ana uwezo mkubwa. Tatizo ni kwamba hajatoa mchango mkubwa wa mabao. Katika mechi 11 za ligi ana asisti moja tu. West Ham sasa wako kwenye hatari ya kushuka daraja na wanahitaji straika huyo aanze kufunga, ingawa kufanya hivyo dhidi ya Arsenal sio kazi rahisi.

10. MADDISON KURUDI NA JAMBO SPURS?

Tottenham Hotspur wana presha kubwa katika vita vya kushuka daraja, lakini ushindi wa hivi karibuni umeongeza matumaini ya kusalia Ligi Kuu England.

Kurudi kwa kiungo wao, James Maddison, kwenye kikosi kumeonekana kuleta hamasa kubwa, licha ya kuwa hajaingia uwanjani tangu apone jeraha kubwa la goti. Kocha Roberto De Zerbi amesema uzoefu na utulivu wa Maddison ni muhimu kwa timu na ikiwa ataingia hata kwa dakika chache dhidi ya Aston Villa inaweza kuwa nguvu mpya kwa Spurs katika mwisho huu mgumu wa msimu kwao.