KATIKA harakati za kuhakikisha safu yao ya ushambuliaji inaendelea kuwa tishio kwa wapinzani, uongozi wa Yanga SC umeamua kukata mzizi wa fitna kwa kukamilisha mpango wa kumuongezea mkataba mshambuliaji wao hatari, Prince Dube.
Hatua hiyo inaonyesha wazi namna mabingwa hao watetezi walivyojipanga kulinda silaha zao muhimu kuelekea misimu ijayo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Yanga imefikia makubaliano rasmi na nyota huyo wa kimataifa kwa ajili ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili zaidi. Uamuzi huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuendelea kuimarisha kikosi na kuhakikisha ushindani unaendelea kubaki upande wao.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, hatua iliyobaki kwa sasa ni kukamilisha taratibu za mwisho za kusaini mkataba huo mpya, huku ikielezwa kuwa kila kitu kinaweza kuhitimishwa muda wowote kabla ya pazia la msimu wa 2025/26 kushushwa rasmi.
Yanga imeonekana kuchukua tahadhari mapema baada ya baadhi ya klabu kuanza kuonyesha nia ya kumtaka mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho.
Uongozi wa Wananchi unaamini kuendelea kumbakiza Dube ni sehemu muhimu ya kudumisha makali ya timu katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeweka wazi kuwa benchi la ufundi limehusika moja kwa moja katika uamuzi huo, likivutiwa na kiwango pamoja na mchango mkubwa wa mchezaji huyo kwenye eneo la ushambuliaji. Dube ameendelea kuwa tegemeo muhimu katika michezo mingi ya Yanga msimu huu.
“Benchi la ufundi limeridhia kabisa aongezwe mkataba, lakini pia namba zake za mabao zimechangia kwa kiasi kikubwa kufanya uamuzi huo kwani ni miongoni mwa wachezaji wenye mchango mkubwa ndani ya Yanga,” kilisema chanzo hicho.
Msimu huu, Prince Dube ameendelea kuthibitisha ubora wake kwa kuwa mmoja wa washambuliaji wenye kiwango cha juu ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hali inayowafanya mashabiki wa Yanga kuwa na matumaini makubwa zaidi kuhusu mustakabali wa safu yao ya ushambuliaji.