Habari za michezo
BMT YAWAAMBIA WAZI YANGA KILICHOIBEBA SIMBA
Vardo
May 11, 2026
10:55 am
KATIBU Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, amefafanua sababu zilizoifanya Simba SC kutwaa tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka 2025, akieleza kuwa mafanikio ya kimataifa ndiyo yalikuwa kigezo kikuu katika mchakato wa upatikanaji wa mshindi wa tuzo hiyo.
Msitha ametoa ufafanuzi huo kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wa Yanga SC waliodai kuwa timu yao ilistahili kuwamo katika kinyang’anyiro hicho kutokana na mafanikio makubwa waliyoonyesha kwenye mashindano ya ndani msimu huu.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Msitha amesema BMT haikuzingatia idadi ya mataji ya ndani pekee, bali ilifanya tathmini ya kiwango cha mafanikio ya klabu katika mashindano ya kimataifa kwa kipindi cha mwaka uliopita.
Amesema lengo la tuzo hizo ni kuthamini timu zinazoiwakilisha vizuri Tanzania nje ya mipaka yake na kuipa nchi heshima kupitia ushindani wa kimataifa.
“Tunaangalia mafanikio ya kimataifa, hatuangalii umefanya nini ndani pekee. Hata kama una makombe 200 ya ndani, ukifanya vibaya katika michuano ya kimataifa huwezi kupata tuzo,” amesema Msitha.
Amewataka wadau wa soka kuelewa vigezo vinavyotumika katika utoaji wa tuzo hizo, akibainisha kuwa washindi wa mwaka huu walionesha kiwango bora katika mashindano ya kimataifa ndani ya kipindi husika.
Usiku wa tuzo za BMT uliofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, uliendelea kuwa wa kihistoria kwa Simba baada ya kutangazwa rasmi kuwa Klabu Bora ya Mwaka 2025 mbele ya wadau mbalimbali wa michezo nchini.
Katika kinyang’anyiro hicho, Simba iliibuka mshindi mbele ya timu ya mpira wa kikapu ya Dar City, huku mafanikio yao yakitajwa kujumuisha kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na kimataifa pamoja na kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.