Habari za michezo
CORAZONE AAMSHA MATUMAINI SIMBA QUEENS KUREJEA LIGI YA MABINGWA AFRIKA
Vardo
May 12, 2026
5:11 pm
KIUNGO wa kimataifa wa Simba Queens, Vivian Corazone, ameweka wazi dhamira yake kuelekea mwisho wa msimu huu kwa kusisitiza kuwa ndoto yake kubwa ni kuirejesha timu hiyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupitia ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL).
Nyota huyo raia wa Kenya ambaye huu ni msimu wake wa tano kuitumikia Simba Queens, amesema ukubwa wa klabu hiyo unamlazimu kupambana kwa nguvu zote kila anapopata nafasi ya kucheza.
Corazone ameweka wazi kuwa hamu yake si kutwaa mataji ya ndani pekee, bali pia kuona timu hiyo ikirejea kwenye ushindani wa kimataifa barani Afrika.
Kwa miaka yote aliyokuwa ndani ya kikosi hicho, Corazone ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kutokana na uzoefu wake mkubwa pamoja na uwezo wake wa kuiongoza timu katika nyakati ngumu.
Ameendelea kubeba matumaini ya mashabiki wengi wanaoamini Simba Queens inaweza kurejea kwenye ubora wake wa kimataifa.
Kwa sasa, Simba Queens wanaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufikia lengo hilo baada ya kuendelea kuongoza msimamo wa WPL wakiwa na alama 43 baada ya kucheza michezo 15. Wapo mbele ya wapinzani wao wakubwa Yanga Princess wenye alama 39 pamoja na mabingwa watetezi JKT Queens walio na pointi 38.
Ingawa tofauti ya alama si kubwa, Simba Queens bado wanashikilia hatima yao mikononi mwao. Kila mchezo uliobaki unaonekana kuwa muhimu katika mbio za ubingwa huku ushindani ukiendelea kuwa mkali kutoka kwa timu zinazowafukuzia kwa karibu.
Corazone amesema hamasa yake kubwa inatokana na kumbukumbu ya msimu wa 2022/23 ambapo alikuwa sehemu ya kikosi kilichoifikisha Simba Queens hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Uzoefu wa kucheza dhidi ya timu kubwa za bara hilo ulimfanya kutambua thamani ya mashindano hayo pamoja na heshima ya kuiwakilisha klabu kimataifa.
Licha ya kuwa tayari ametwaa mataji mawili ya ligi akiwa na Simba Queens, Corazone anaamini safari bado haijaisha. Kwa mtazamo wake, msimu huu unaweza kuwa wa kipekee zaidi ikiwa timu hiyo itatwaa ubingwa na kupata tiketi ya kurejea tena Afrika, jambo ambalo linaweza kuandika historia mpya kwa Simba Queens katika soka la wanawake barani humo.