Habari za michezo
NIMEWAFUNDISHA, NAWAHESHIMU LAKINI PRESHA NI YAO, JULIO AWAPANDISHA JOTO SIMBA
Vardo
May 12, 2026
4:57 pm
KOCHA wa Mashujaa FC, Jamhuri Kihwelo, ameongeza presha kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC baada ya kueleza namna alivyojipanga kiakili kuhakikisha anawavuruga wapinzani wao katika pambano hilo muhimu.
Mashujaa watakuwa nyumbani kwenye mchezo huo utakaopigwa Mei 14 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, huku presha kubwa ikionekana kuhamia kwa wageni wanaosaka ushindi muhimu katika mbio za ligi.
Kihwelo, ambaye aliwahi kuitumikia Simba kama kocha msaidizi, amesema ana heshima kubwa kwa klabu hiyo kutokana na historia yake ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi, lakini hilo halimzuii kupambana kutafuta matokeo mbele ya mashabiki wake.
” Simba ni moja ya timu kubwa nchini na hatuwezi kuidharau, lakini kama kocha wa Mashujaa nina wajibu wa kuhakikisha timu yangu inapambana kupata ushindi nyumbani Kigoma,” amesema.
Kocha huyo pia ameweka wazi kuwa hafungi milango ya uwezekano wa kupoteza mchezo huo, akisisitiza kuwa katika soka matokeo yoyote yanaweza kutokea, lakini akaeleza kuwa presha kubwa zaidi ipo upande wa Simba.
Kauli ya Kihwelo imeonekana kama mbinu ya kisaikolojia inayolenga kuwabebesha mzigo Wekundu wa Msimbazi kabla ya mchezo huo mgumu, hasa ikizingatiwa kuwa Mashujaa wataingia wakiwa hawana cha kupoteza mbele ya wapinzani wao wenye uzoefu mkubwa.
Amesisitiza kuwa kwake kupoteza dhidi ya Simba haitakuwa habari kubwa, lakini ikiwa Mashujaa wataibuka na ushindi dhidi ya Simba, basi hilo litakuwa gumzo kubwa nchini kutokana na ukubwa wa mchezo huo na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.