Habari za michezo

FABREGAS AIVUSHA COMO ULAYA, VITA YAENDELEA SERIE A NA LIGI KUBWA ULAYA

Vardo May 12, 2026 9:44 am

COMO, PARIS: KOCHA Cesc Fabregas ameendelea kuandika historia mpya ndani ya soka la Italia baada ya kuiwezesha Como 1907 kufuzu kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Hellas Verona katika mchezo wa Serie A uliochezwa, Marcantonio Bentegodi.

Ushindi huo umeifanya Como kujihakikishia nafasi ya kucheza angalau UEFA Conference League msimu ujao huku timu hiyo ikiendelea kushikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa Serie A ikiwa na tofauti ya pointi 10 dhidi ya Atalanta walio nafasi ya saba.

Katika mchezo huo, Como yenye pointi 65 katika nafasi ya sita walionyesha ubora mkubwa wa kumiliki mpira lakini walilazimika kusubiri hadi dakika ya 71 ndipo mshambuliaji Anastasios Douvikas alipofunga bao pekee la ushindi, ambalo pia lilikuwa la 13 kwake msimu huu wa 2025/26.

Katika raundi mbili ambazo zimesalia za ligi hiyo kwa sasa Como inapambana kumaliza katika nafasi nne za juu ili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitu ambacho kinawezekana kulingana na utofauti wa pointi uliopo baina yao na timu zilizopo nafasi hizo.

AS Roma ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 67 ambazo ni sawa na AC Milan ambayo ipo nafasi ya nne huku Juventus ikiwa na pointi 68 katika nafasi ya tatu, Napoli ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 70.

Katika mechi mbili zilizosalia Como itacheza dhidi ya Parma na Cremonense ambayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja.

Akiongelea mafanikio hayo, Fabregas hakuficha furaha yake kutokana na mafanikio hayo makubwa aliyoyapata ndani ya kipindi kifupi tangu aipandishe Como hadi Serie A miaka miwili iliyopita.

“Nina furaha sana na najivunia sana timu hii. Miaka miwili iliyopita siku kama ya leo tulipanda Serie A na leo tunafuzu kucheza Ulaya. Hiki ni kitu kikubwa sana kwa klabu, mashabiki na kila mtu anayehusika,” anasema Fabregas.

Nyota huyo wa zamani wa FC Barcelona na Arsenal FC alisema mafanikio hayo ni matokeo ya ukuaji mkubwa wa timu ndani na nje ya uwanja, huku akisisitiza kuwa siku hiyo itaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu na mashabiki wa Como.

“Watu wote wamekua pamoja na timu hii. Mashabiki, viongozi na wachezaji wameonyesha moyo mkubwa sana. Hii ni siku ambayo naamini hata baada ya miaka 20 bado watu wataikumbuka,” anasema.

Fabregas pia alizungumzia presha kubwa iliyopo kwenye soka la kisasa, akisema maendeleo ya mitandao ya kijamii yameongeza kasi ya hukumu na matarajio kwa makocha pamoja na wachezaji.

Kwa upande wa Ligi ya Ufaransa, mbali na Psg kuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya tano kuna vita ya timu sita katika kuwania nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Ni PSG na Lens ndio zenye uhakika wa kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, kuna vita kwa timu tano tofauti ambazo ni Lille yenye pointi 61 ikiwa nafasi ya tatu, Lyon yenye pointi 60 ikifuata, Rennes pointi 59, Marseille (56) na Monaco 54.

Timu tatu za juu kwenye Ligi ya Ufaransa ndio zinajikatia tiketi ya moja kwa moja kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao huku ile ambayo itashika nafasi ya tatu ikianzia mchujo, timu itakayomliza msimu ikiwa nafasi ya tano itacheza Europa League huku nafasi ya sita ikiwa Europa Conference League.

Kwa upande wa Hispania ni Barcelona, Real Madrid, Villarreal na Atletico Madrid zenye uhakika msimu ujao kucheza Ligi ya Mabingwa bado vita ipo kwa Real Betis na Celta Vigo ambao wanapigania nafasi ya tano, Hispania na England wao wanaingiza timu tano katika michuano hiyo kutokana na klabu zao kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.Katika Ligi ya Ujerumani, Bayern Munich, Dortmund na RB Leipzig zinauhakika wa kucheza michuano ya Ulaya huku vita ikibakia kwa Stuttgart na Hoffenheim wote wanapointi 61 kila mtu anatolea macho nafasi ya nne huku kukisaliwa na raundi moja ya ligi.

DAKIKA 720 BILA HAT TRICK, MASTRAIKA WATAJA SABABU