Habari za michezo
DAKIKA 720 BILA HAT TRICK, MASTRAIKA WATAJA SABABU
Vardo
May 12, 2026
9:36 am
WAKATI zikibaki raundi nane sawa na dakika 720 kumalizika kwa Ligi Kuu msimu wa 2025-2026, maajabu yameonekana kwa kukosa mchezaji aliyefunga mabao matatu katika mchezo mmoja (hat trick), ikilinganishwa na msimu uliopita.
Kwa sasa ushindani umeonekana katika vita ya ubingwa, nafasi nne za juu na zile zinazopambania kubaki salama na kukwepa kushuka daraja ukifanya utamu wa ligi hiyo kunoga.
Kwa sasa swali linalotawala katika vichwa vya wadau na mashabiki wa soka nchini ni namna ukame wa ‘hat trick’ ulivyotawala kwa mastaa wa Ligi Kuu kwa timu zote kuanzia vinara Yanga hadi KMC inayoburuza mkia.
Pia kasi ya ufungaji mabao imeonekana kuwa ndogo kwani katika raundi 22 iliyochezwa hadi sasa, kinara wa mabao Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC ameweka 10 tu huku Prince Dube (Yanga) akiwa na tisa, Fabrice Ngoy wa Namungo akiwa na nane.
Katika msimu uliopita, hadi kufikia mzunguko wa 22 ilishuhudiwa wachezaji watano waking’ara na ‘hat trick’ wakiwa ni Meddie Kagere (Namungo), aliyefunga mabao matatu dhidi ya KenGold katika ushindi wa 5-0.
Wengine waliofanya hivyo ni Jean Charles Ahoua (Simba) aliyeng’ara mechi mbili tofauti akifanya hivyo dhidi ya Dodoma Jiji kwenye ushindi wa 6-0, kisha kutakata dhidi ya Pamba Jiji katika ushindi wa 5-1.
Pia staa wa Simba, Steven Mukwala aliingia katika orodha hiyo wakati Mnyama akishinda 3-0 dhidi ya Coastal Union, huku Prince Dube akiwaka wakati Yanga ikiizamisha KenGold mabao 6-1.
Pacome Zouzoua wa Yanga hakuwa mbali na wababe wa hat trick alipofanya hivyo katika mchezo dhidi ya Fountain Gate alipoiongoza timu hiyo kushinda mabao 5-0 ikiwa raundi ya 16.
Straika wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh amesema ugumu wanaopitia washambuliaji haswa kukabwa na mabeki ndio inawapa nafasi winga na viungo kutawala kwenye ufungaji mabao.
“Mpira wa kisasa ndio unaleta mabadiliko haya, unapopangwa namba tisa unazungukwa na mabeki wengi, hali hii inafanya wale waliopo pembeni au nyuma yako kutumia nafasi kufunga mabao.
“Njia mbadala ya kumalizana na changamoto hii kwa sisi washambuliaji ni kubadilishana namba, yaani usikae eneo moja kusubiri mpira bali unaweza kupanda na kushuka kutafuta mpira na kufunga,” amesema nyota huyo.
Kwa upande wake nahodha wa zamani wa Yanga, Simba, Majimaji na Taifa Stars, Willy Martin, amesema msimu huu imekuwa tofauti na matarajio yao akieleza kuwa wanachobaini ni ubinafsi kwa wachezaji.
“Kwanza wanaofunga siyo washambuliaji ni aidha winga au viungo, sisi zamani tulikuwa na wakali wa nyavu kama Said Mwamba, Peter Tino na Abeid Mziba, lakini walikuwepo watengeneza mabao kama Edibil Lunyamila.
“Kwanza wanaofunga siyo washambuliaji ni aidha winga au viungo, sisi zamani tulikuwa na wakali wa nyavu kama Said Mwamba, Peter Tino na Abeid Mziba, lakini walikuwepo watengeneza mabao kama Edibil Lunyamila,” amesema.