CHORILA MAKOCHA WA NGUMI TUNAISHI MAISHA MAGUMU
KATIKATI ya mitaa ya Manzese Tiptop, eneo la Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, kuna ukumbi mdogo unaobeba ndoto kubwa za vijana wanaopambana kubadili maisha yao kupitia mchezo wa ngumi.
Ndani ya Chorila Boxing, kila tone la jasho, kila pigo la glove na kila zoezi ni sehemu ya safari ya matumaini kwa vijana wanaotafuta mafanikio.
Safari hiyo inaongozwa na kocha Ramadhani Mustafa maarufu Chorila, ambaye ameigeuza klabu hiyo kuwa zaidi ya sehemu ya mazoezi, ni mahali pa malezi, nidhamu na kutengeneza maisha kwa vijana wengi wa mitaani.Soka laa Bongo ilifunga safari hadi kwenye gym hiyo na kufanya mahojiano na kocha huyo kuhusu safari yake ya ukocha akielezea changamoto mbalimbali zinazowakumba ikiwemo ishu ya mikataba na makocha kutopewa thamani inayostahili.
SAFARI YAKE
Chorila anaanza kusimulia historia yake kwa utulivu mkubwa. Anasema mapenzi yake kwenye mchezo wa ngumi yalianza tangu akiwa mtoto mdogo.
“Nikiwa darasa la nne tayari nilikuwa napenda sana ngumi. Nilikuwa nikiona mabondia wakipigana na mimi nikajikuta natamani siku moja niwe kama wao,” anasema.
Alianza kama bondia wa ridhaa mwaka 2014 kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa. Hata hivyo, maisha ya familia na changamoto mbalimbali vilimfanya abadili uelekeo na kuingia kwenye ukocha.
“Mchezo wa ngumi haukunilipa nilivyoona hivyo sikucheza sana nafikiri nilicheza msimu mmoja tu nikaona niachane na ngumi nifanye mambo mengine lakini nisiache kabisa,” anasema Chorila na kuongeza;
“Niliona nina uwezo wa kuwasaidia vijana wengine. Mimi nilishapitia maumivu yote ya ngumi, hakukuwa na hela nikasema kwa nini nisiwe mwalimu wa kuwainua wale wanaotoka mazingira magumu kama yangu,” anasema.
Kocha huyo kwa sasa ana gym yake iitwayo Chorila Boxing ina zaidi ya mabondia 20 wanaofanya mazoezi kila siku. Wengi wao ni vijana wa kawaida wanaotoka mitaa ya Dar es Salaam na maeneo mengine wakiamini ndoto zao zinaweza kutimia kupitia ngumi.
NIDHAMU NDIYO MSINGI WA BONDIA
Katika mazungumzo yake, jambo ambalo Chorila analisisitiza zaidi ni nidhamu. Anaamini hakuna bondia anayeweza kufika mbali bila kuwa na nidhamu ya ndani na je ya ulingo.
Kwa mujibu wake, changamoto kubwa inayowakumba mabondia wengi ni kubadilika wanapoanza kupata umaarufu kidogo na hapo ndipo wanapopotea kwenye karia hiyo.
“Bondia akishaanza kujulikana kidogo tu, anaanza kuona ameshakuwa mkubwa kuliko mwalimu wake. Hapo ndipo matatizo yanaanza,” anasema .
Anaeleza baadhi ya mabondia huanza kukwepa mazoezi, kuchelewa kambini au hata kupuuza maelekezo ya walimu wao wakiamini tayari wamefikia mafanikio fulani.
“Ngumi siyo nguvu tu. Nidhamu ndiyo kila kitu ukikosa nidhamu hata kama una kipaji kikubwa, huwezi kufika popote,” anasisitiza.
“Ukiona bondia hana nidhamu, wakati mwingine unalazimika kumpumzisha kabisa. Anaweza kukaa hata miezi mitatu bila kushiriki mazoezi ili ajifunze,” anasema.
UCHUNGU WA KULEA BONDIA
Mbali na changamoto ya nidhamu, Chorila anasema kuna tatizo jingine linaloumiza walimu wengi wa ngumi nchini mabondia kuwakimbia walimu wao baada ya kupata mafanikio.
Anaeleza kuwa makocha wengi huanza na vijana wakiwa hawana chochote, huwatengeneza kuanzia kwenye nidhamu kwa sababu wengi wanatokea mitaani wakiwa watukutu.
“Unamlea bondia kwa miaka mingi, kuna wakati unampa chakula hadi nauli, unampigania hadi anaanza kupata jina, halafu siku moja anakwambia anataka kocha mwingine mkubwa zaidi inauma sana,” anasema.
Kocha huyo anaongeza kuwa tatizo hilo linaongezeka kutokana na mabondia wengi kutotaka kusaini mikataba rasmi na walimu wao.
“Wengi wanaogopa mikataba kwa sababu wanafikiri watabanwa. Lakini mikataba ndiyo inalinda pande zote mbili,” anasema.
Anaamini mfumo bora wa mikataba unaweza kusaidia kukuza taaluma ya ngumi nchini na kuondoa migogoro isiyo ya lazima kati ya walimu na mabondia.
MISHAHARA
Anasema asilimia 70 ya makocha wa ngumi hawana mishahara kama ilivyo kwenye soka na michezo mingine bali wanategemea pambano la bondia wake ndio apate chochote cha kujikimu.
“Makocha wanalipwa hadi bondia anapopata pambano sasa inategemea kwa wale mabondia wakubwa kidogo makocha wao wanapata kitu lakini huku kwetu unapata elfu 30,” anasema na kuongeza
“Bondia akipata pambano analipwa 100,000 hapo mnaandikishana yeye anachukua elfu 70,000 na wewe unapata elfu 30,000, sasa kama bondia akikaa mwaka mzima bila ya pambano hatuambulii chochote,” anasema Chorila
FUNZO
Kocha huyo anasema yeye amejifunza kupitia mabondia aliowahi kuwasimamia hapo kabla hivyo kwa sasa mabondia wawili ameingia nao mkataba rasmi.
“Tumejifunza kwa sababu zamani ilikuwa tunachukuliana ile ya urafiki lakini kwenye Gym yangu nina mikataba na mabondia wawili na wengine chipukizi niko kwenye harakati hizo.”
MIPANGO YA TPBCA
Anaamini changamoto hizo zitamalizwa hivi karibuni kutokana na mipango ya Chama cha makocha wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania (TPBCA) ya kusaidia makocha.
“TPBCA mwaka huu ina mipango mingi mojawapo ni hilo la makocha kuna mambo yanawekwa sawa tunaamini kama litafanikiwa makocha na sisi angalau itatusaidia.”
MLO WA MABONDIA
Mbali na mazoezi, Chorila anaamini lishe bora ndiyo silaha nyingine muhimu kwa bondia, anasema bondia anatakiwa kula vyakula vya asili vinavyoongeza nguvu mwilini.
“Bondia anatakiwa ale ugali, dagaa, maharage, mboga za majani na kunywa maji mengi. Hivi vitu vinajenga mwili wa bondia na kuwa n uzito unaoendana na ngumi,” anasema
Kwa upande wake, anaamini mabondia wengi wa sasa wanaharibu afya zao kwa kula vyakula visivyo sahihi na kutegemea zaidi vyakula vya haraka.
“Ngumi zinahitaji stamina kubwa. Ukila hovyo huwezi kudumu ulingoni wenzetu nje wanafuatilia sana suala la mlo lakini sisi kutokana na changamoto ya kifedha ndio tunashauriwa kula vyakula vinavyoongeza nguvu,” anasema.
Mazoezi katika Gym yake hufanyika mara mbili kwa siku asubuhi na jioni. Anasema bondia anatakiwa kuwa fiti muda wote badala ya kusubiri pambano likaribie ndipo aanze kujiandaa.
Hata hivyo, anakiri kuwa changamoto ya uchumi huwafanya baadhi ya mabondia wake kushindwa kupata lishe bora wanaporudi nyumbani.
“Wapo wanaokuja mazoezini vizuri unawapa mazoezi yanayozindatia kilo zao lakini wakirudi nyumbani hakuna chakula bora. Hapo ndipo changamoto kubwa ilipo,” anasema.
VIPAJI VINGI
Licha ya changamoto zote, Chorila anaamini Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji vya ngumi vinavyoweza kufanya vizuri kimataifa iwapo vitapata sapoti kubwa.
Anazitaja kampuni na mapromota mbalimbali wanaojitahidi kuendeleza mchezo huo, lakini anaamini bado kuna haja ya kuwekeza zaidi kwa vijana wa chini ambao hawajajulikana.
“Wadhamini wasikae kusubiri majina makubwa pekee. Huku chini kuna vijana wengi sana wenye vipaji vya ajabu,” anasema.
Anasema baadhi ya mabondia wake wameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza mapambano ya kimataifa. Anamtaja bondia Juma Zenga kama mmoja wa vijana anaowapa matumaini makubwa.
“Ninaamini kabisa kuna siku vijana wetu wataenda kupigana nje na kuiletea Tanzania heshima kubwa,” anasema.
KUHUSU NAHODHA
Akimzungumzia nahodha wa Gym hiyo, Pius Mpenda, Chorila anaamini kuna mengi makubwa watu wayatarajie kutoka kwa bondia huyo mwenye rekodi ya aina yake kimataifa.
“Nafikiri watu waendelee kumsapoti kuna mengi makubwa yanakuja mbeleni, Mpenda ni bondia mzuri na naimani ndani ya miaka mitano atakuja kuiheshimisha Tanzania,” anasema Chorila.
Ni mmoja wa mabondia wanaoshikilia mikanda iliyotoka WBC na rekodi ya kucheza mapambano 13, akishinda 10 kati ya hayo matano ameshinda kwa Knockout na amepigwa mara tatu kati ya hizo moja ni kwa Knockout.
NDOTO ZAKE
Chorila anasema bado ana ndoto kubwa kwenye mchezo huo. Mbali na kutamani kuona mabondia wake wakifanikiwa, anaamini siku moja atakuwa na gym ya kisasa yenye vifaa vya kiwango cha kimataifa.
“Tunahitaji vifaa vizuri vya kujenga nguvu, akili na stamina za mabondia. Hapo ndipo tunaweza kuzalisha mabondia wakubwa duniani,” anasema.
Pia anaendelea kusomea masuala ya ukocha ili kuongeza ujuzi wake na kupata vyeti vya kimataifa.
Anasema angependa watoto wake waingie kwenye mchezo wa ngumi, lakini hatawalazimisha.
“Kikubwa kwanza waweke elimu kichwani. Ngumi ni kitu ambacho lazima mtu akipende mwenyewe kutoka moyoni na sio kulazimishwa eti kwa sababu baba alifanya,” anasema.
PESA KUBWA
Kocha huyo anasema pesa kubwa aliyowahi kuipata kwenye ngumi ni Sh 500,000 “Hiyo ndiyo fedha niliyopata kubwa lakini nyingine ndiyo kama nilivyokwambia elfu 30,000.”