Habari za michezo

MASHUJAA WAMEINGIA KWENYE HESABU ZA SIMBA, MATOLA ATOA ONYO

Vardo May 13, 2026 9:08 am

WAKATI ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukiendelea kupamba moto, benchi la ufundi la Simba SC limefafanua sababu za kutokwenda mapema Kigoma kuelekea mchezo wao dhidi ya Mashujaa FC, likieleza kuwa changamoto ya viwanja vya mazoezi pamoja na ratiba ngumu ya mechi ndiyo imechangia uamuzi huo.

Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema Mkoa wa Kigoma una uhaba wa viwanja vinavyoweza kutumiwa kwa mazoezi ya timu kubwa, jambo lililowalazimu kupanga safari yao kwa kuzingatia muda wa kufanya mazoezi rasmi kwenye uwanja wa mchezo.

Amesema kwa mujibu wa kanuni za mashindano, timu inaruhusiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla ya mchezo, hivyo wakaona ni bora kusafiri kwa muda sahihi kuliko kuwahi na kukosa mazingira mazuri ya maandalizi.

“Ukiangalia kijiografia unajua Mkoa wa Kigoma hakuna viwanja vingi vya mazoezi, hivyo tumepanga kwenda siku moja kabla ili kama sheria inavyoturuhusu tuweze kufanya mazoezi kwenye uwanja ambao tutachezea,” amesema Matola.

Matola ameongeza kuwa msongamano wa ratiba ya ligi pia umeifanya Simba kushindwa kukaa muda mrefu sehemu moja, kutokana na timu kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi.

“Tukienda mapema sana tunapata tabu ya viwanja vya mazoezi, pia muda ni mdogo kwa sababu kila baada ya siku mbili kuna mechi, hivyo huwezi kwenda kukaa siku mbili sehemu moja,” amesema.

Pamoja na changamoto hizo, Matola amesema kikosi hicho kimejiandaa vizuri kwa ajili ya kusaka ushindi dhidi ya Mashujaa FC, huku kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi kukiongeza matumaini ndani ya timu.

Amesisitiza kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na kiwango kizuri kinachoonyeshwa na Mashujaa FC chini ya kocha wao mpya, Julio, ambaye tangu ajiunge na timu hiyo bado hajapoteza mchezo wowote.

“Kwetu sisi haitatusumbua kwa upande wa kiufundi, lakini haitakuwa mechi rahisi. Mashujaa FC ni washindani wazuri kwa sasa, wamerudi vizuri na wana kocha mpya Julio ambaye ni mshindani, na tangu amefika hajawahi kupoteza,” amesema Matola..

HALI YA KIKOSI YANGA YAFICHULIWA KABLA YA MECHI CHORILA MAKOCHA WA NGUMI TUNAISHI MAISHA MAGUMU