Habari za michezo
DODOMA JIJI YAPANIA KUIVURUGA YANGA KWENYE MBIO ZA UBINGWA
Vardo
May 13, 2026
12:10 pm
BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC, leo anaingia uwanjani ugenini kupambana na Dodoma Jiji, katika mechi yenye hesabu kali.
Katika mchezo huu, kutakuwa na mbio za kuusaka ubingwa, sambamba na kujiimarisha kwenye nafasi na kuwa salama.
Yanga chini ya kocha wa muda, Abdihamid Moalin atakayekuwa anaiongoza timu hiyo kwenye mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara, ana kazi ya kuendeleza rekodi ya ushindi kwenye Uwanja wa Airtel uliopo Singida.
Yanga ina hesabu moja tu ikitaka kushinda mbele ya Dodoma ili kujiweka salama katika mbio za kwenda kulifuata taji la tano mfululizo ikikutana na wenyeji wao ambao wamehamia kwa muda mkoani Singida baada ya uwanja wao wa Jamhuri jijini Dodoma kufungiwa.
Dodoma yenye pointi 29 ikiwa nafasi ya nane, inahitaji ushindi ili kupanda nafasi moja hadi ya saba kwa kufikisha pointi 32.
Yanga inakwenda kukutana na Dodoma ambayo haina historia ya kupata hata sare kwenye mechi 11 walizokutana kwenye ligi.
Katika mechi tano za mwisho, Yanga imeangusha pointi mbili tu ilipopata sare ya ugenini dhidi ya Simba, kisha ikashinda mechi nne, ambapo habari njema kwao ni kurejea kwa wachezake wawili kiungo Mudathir Yahaya aliyemaliza adhabu ya kusimamishwa mechi tatu na kamati ya usimamizi wa ligi.
Mwingine ni beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye aliumia akiwa Zanzibar kwenye mechi za Kombe la Muungano.
Kocha Moalin akizungumzia mchezo huo amesema haitakuwa rahisi dhidi ya Dodoma ambao wamekuwa wakitoa ushindani timu hizo zinapokutana licha ya kwamba mabingwa hao wamekuwa wakishinda.
“Utakumbuka kwenye mchezo wa kwanza tukiwa nyumbani walianza kutufunga lakini tulikuwa imara tukasawazisha na kushinda, Dodoma ni timu nzuri hutakiwi kwenda kukutanan nayo ukiona kama itakuwa mechi rahisi,” amesema Moalin atakayekuwa anaanza mechi yake ya kwanza ugenini.
“Tunataka kucheza kwa ubora mkubwa, wakati kama huu sio salama sana kuangusha pointi, hatutaki kitu kama hicho kitokee, tumesafiri na wachezaji wote muhimu na wako sawasawa, tupo tayari kwa mchezo.”
Dodoma itatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Prince Dube ambaye ndiye kinara wa ufungaji kikosini hapo akifunga mabao tisa, kiungo Allan Okello ambaye ni kinara wa kutengeneza pasi za mwisho pale Yanga akiwa nazo saba.
Changamoto kubwa ya Dodoma ni kwamba imeruhusu mabao 21 wakati ikifunga 19, ikionyesha kwamba ukuta wao unatakiwa kuwa makini mbele ya Yanga ambayo ndani ya mechi saba imefunga mabao 19.
Dodoma itategemea nguvu ya mshambuliaji wake William Edgar ambaye ni kinara wa kufunga kwenye timu hiyo akiwa na mabao sita ambaye pia ndiye aliyemtungua kipa wa Yanga, Djigui Diarra kwenye mchezo wa mwisho walipokutana na mabingwa hao walishinda kwa mabao 3-1.
Kocha wa Dodoma, Amani Josiah, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana na Yanga wakitambua kwamba wanakwenda kukutana na timu yenye wachezaji bora lakini wanataka kutumia udhaifu wao kutafuta pointi.
“Tunakwenda kwenye mchezo mgumu, mara ya mwisho tulipokutana kwao, tuliwabana vizuri lakini baadaye tulipopata bao kina makosa tulitafanya yakatugharimu na kupoteza mchezo, Yanga ni wazuri wana wachezaji wenye uzoefu lakini haina maana kwamba haifanyi makosa, tutakwenda kutumia makosa yao,” amesema Josiah.